Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike amezipongeza Taasisi za kidini ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za kijamii ikiwemo Elimu hatua ambayo imeongeza kasi ya Maendeleo nchini.
Ametoa pongezi hizo leo wakati wa Mahafali ya kuwaaga Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki (TMCS) yaliyofanyika katika Viwanja vya Hospitali ya Kanda ya Bugando.
"Serikali itaendelea kuthamini mchango wenu, tangu kuanzishwa kwa Vyuo hivi vimewanufaisha Watanzania wengi na Serikali kwa ujumla kwani watu wenye afya ni mtaji muhimu wa Maendeleo kwa Taifa." amesema Ngusa.
Samike, amewakumbusha Wahitimu hao kuendeleza Taswira ya Ukatoliki waliotoka nayo vyuoni ili kuwa mfano wa kuigwa ndani ya Jamii huku wakibuni mbinu mbalimbali za kujiajiri wenyewe kutokana na Serikali kutoa fursa nyingi za mikopo.
Aidha, amewataka Wataalamu wa dawa kuleta mageuzi chanya watakapoajiriwa kutokana na changamoto iliyopo sasa ya dawa nyingi kuchina kwenye Vituo vya afya hali inayosababishwa na uagizaji usiozingatia takwimu sahihi.
Mlezi wa Umoja wa Wanafunzi hao Padri Renatus Mashishanga amesema wamekuwa na mafanikio mbalimbali yakiwemo kufanya matendo ya huruma kwa kuwatembelea na kuwapa mahitaji muhimu wafungwa kwenye Gereza la Butimba na watoto waishio katika mazingira magumu.
Pia, Katibu Tawala amewakumbusha Wahitimu hao kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika nchini kwa wale walio ndani ya mipaka ya Tanzania mnamo Agosti 23 mwaka huu.
Mahafali hayo ya Wahitimu Wanafunzi Wakatoliki yamewajumuisha wanaosomea Udaktari, Uuguzi, Ufamasia, Utaalamu wa Maabara, na Utaalamu wa Viungo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.