Licha ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi aina ya Corona (COVID-19) kupungua wananchi Mkoani Mwanza wameombwa kuendelea kuchukua tahadahari huku shirika la AGPAHI likitoa msaada wa vifaa vya kupimia joto kwa ajili ya uchunguzi wa awali wa ugonjwa huo.
Ambapo AGPAHI imekabidhi jumla ya mashine 100 zenye thamani ya milioni 25 kupitia ufadhili wa taasisi ya CDC kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambavyo vimepokelewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmanuel Tutuba.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmanuel Tutuba, amemshukuru Mungu kuwa kwa sasa Mkoa huo, maambukizi ya Corona yamepungua lakini wanaendelea kusisitiza watu wote waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Tutuba anasema, endapo kutakuwa na mgonjwa au mtu mwenyewe anayejihisi kuwa na dalili mbalimbali za awali za ugonjwa huo asisite kwenda kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili wataalamu waendelee na vipimo na hatimaye kumpatia matibabu.
Pia anasema,wameendelea kuwasisitiza watoa huduma kuendelea kutoa huduma bila unyanyapaa huku wananchi wakitakiwa kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono na maji tiririka, sabuni na kutumia vitakasa mikono na kuendelea kuzingatia maelekezo mbalimbali ikiwemo kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine.
Tutuba alilishukuru shirika hilo pamoja na wadau wengine wanaounga mkono kwa kuwezesha vifaa mbalimbali wanavyovitoa ambapo walikuwa na kiu kubwa sana kwani katika vikao mbalimbali walikuwa wakiongelea namna ya kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini nani mwenye dalili za awali kupitia joto linalozidi kiwango ili kusudi aendelee kupata huduma nyingine za kimatibabu endapo atakuwa ameshukiwa kuwa na ugonjwa huo.
"Nitumie fursa hii kuwashukuru sana kwa msaada huu ambao mmeutoa wakati muafaka kwani bado vinahitajika,kama sekretarieti ya Mkoa tuna ahidi kwamba mashine hizo zitagawiwa kwenye maeneo yote ambayo Mkuu wa Mkoa ameisha yaainisha na zitatumika kwa uangalifu na kwa mahitaji yaliyokusudiwa,"anasema Tutuba.
Kwa upande wake Meneja Mipango wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa Dkt.Nkingwa Mabelele anasema wamekuja kukabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya milioni 25 ambavyo vitatumika kupima joto la mtu ili kubaini mwenye joto la juu ambaye inawezekana akawa na maambukizi ya virusi vya Corona.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.