Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima ameiasa jamii kuachana na tabia hatarishi zinazochochea Maambikizi ya VVU/UKIMWI ili kuepukana na athari za janga hilo.
Malima ametoa rai hiyo leo (Disemba 01, 2022) kwenye viwanja vya Mirongo Jijini Mwanza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kimkoa kwenye viwanja hivyo.
"Kwa takwimu hizi za Maambukizi ya Asilimia 7.2 Mkoani kwetu ambayo ni zaidi ya Asilimia 4 ya Kitaifa inaonesha hali ya Maambukizi kwa Mwanza kuwa bado yapo juu sana hivyo ni lazima tulifanyie kazi suala hili hususani kuwakinga na janga hili watoto wetu ambao ni Taifa la kesho." Malima.
Aidha, ametoa wito kwa wenye Maambukizi ya VVU/UKIMWI kutumia dawa za kufubaza maambukizi ili kuendelea kuzalisha uchumi wao kwa kujitafutia kipato kwa kukuza mitaji inayosaidia kuboresha maisha yao.
Hata hivyo, ametoa wito kwa mashirika yote Mkoani humo kushirikiana na serikali katika kukidhi matakwa ya kitaalamu na miongozo ya Wizara ya Afya katika kuhudumia Wananchi na amezitaka Halmashauri kupeleka nguvu kwenye afua za kudhibiti maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa ICAP nchini ndugu Michael Kalunga amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali kupitia kutoa msaada wa vifaa tiba kuhakikisha wanafikia malengo ya kusaidia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi waweze kufahamu hali zao.
Yasin Ally, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini amesema Shirika hilo linafanya jitihada katika kuhakikisha wanakemea masuala ya ukatili wa kijinsia kama Ubakaji wenye matukio 479, matukio 1115 ya Mimba za utotoni na 1044 ya Ulawiti mkoani humo ili kuwafanya watoto waweze kustawi.
Akisoma risala ya Maadhimisho hayo, Joseph Kiarata amesema huduma zisizo na vikwazo kwa watoto na jamii kwa ujumla ndiyo lengo la Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii bila ubaguzi.
"Katika 2016 hadi 17 Mkoa wa Mwanza uliongeza maambikizi ya VVU/UKIMWI kwa asilimia 7 lakini Serikali inaendelea kufanya afua mbalimbali za kusaidia kufuta maambukizi mapya kama matumizi ya kondomu, kukemea matumizi ya dawa za kulevya, ndoa za utotoni, ulawiti na Ubakaji na kuhudumia wanaoishi na VVU/UKIMWI.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.