SKIMU YA UMWAGILIAJI KUSAIDIA KUONGEZA UZALISHAJI MAZAO BUCHOSA
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava leo tarehe 06 Oktoba, 2024 amezindua mradi wa skimu ya umwagiliaji iliyojengwa kwa Tshs. Bilioni 2. 4 kupitia tume ya taifa ya umwagiliaji kwenye kijiji cha Sukuma kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Akizungumza na wananchi wa Sukuma, Magurukenda na maeneo ya jirani, ndugu Mnzava ameipongeza serikali kwa kutekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo na amebainisha kuwa itawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji kwa kufanya shughuli hizo katika kipindi chote cha mwaka pasipo kusubiri mvua.
Ametumia pia wasaa huo kuwaondoa hofu wananchi kwamba mradi huo sio kwa ajili ya wawekezaji na katika hilo amewahakikishia kuwa mradi huo ni kwa ajili ya wananchi na kwamba serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuwainua wananchi wake kiuchumi.
"Mradi huu ni kwa ajili ya wananchi sio wawekezaji, naomba mpuuze maneno na minong'ono inayosema kwamba mradi huo umetekelezwa kwa ajili ya wawekezaji tumieni fursa hii kuongeza uzalishaji kwenye mazao ya chakula, matunda na mbogamboga." Amesema Kiongozi wa mbio za Mlmwenge
Aidha, Mwenge wa uhuru umezindua madarasa 2 na matundu 6 ya vyoo katika shule ya awali na msingi Nyehunge iliyotekelezwa na serikali kwa Tshs. milioni 55.8 kupitia mradi wa GPE LANES kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye Zahanati ya Nyakasungwa ambapo Milioni 250 za mapato ya ndani yakijenga majengo ya OPD na maabara.
Halikadhalika, mwenge wa uhuru umezindua mradi wa maji kwenye kijiji cha Kasela wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni moja kwa siku wenye thamani ya Milioni 218 ambapo kiongozi wa mbio hizo amewapongeza wasimamizi (RUWASA) kwa kuongeza hali ya upatikanaji wa maji safi kutoka 10% hadi 85%.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.