Mamlaka ya usafiri wa Nchi kavu na majini (SUMATRA) imetoa mafunzo kwa wafanyabiashara na wamiliki wa magari ya kubeba abiria wa Mkoa wa Mwanza na Mikoa ya jirani ili kuboresha mfumo wa usafirishaji na kutatua changamoto za misongamano ya daladala mijini.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo, Meneja leseni wa kanda ya ziwa Leo Ngowi alisema, Mkoa wa Mwanza una daladala 3,240 kati ya hizo 2,800 zinauwezo wa kubeba abiria 20.
Mikoa mingine ni Geita wenye daladala 950 kati ya hizo 530 ndizo zenye uwezo wa kubeba abiria 20 na Mkoa wa Mara una daladala 1,360 zenye uwezo wa kubeba abiria ni 1300.
Mkurugenzi wa Sumatra Nchini Gilliard Ngewe alisema wameamua kufanya mafunzo hayo ili kuwaandaa wamiliki kisaikolojia pindi mabasi makubwa ya abiria yatakapo wasili, kutatua changamoto za msongamano wa daladala mijini na kupunguza hewa ya ukawa inayotokana na daladala.
“Licha ya kupunguza msongamano barabarani lakini pia madereva na makondakta watapata ajira kwa kulipwa stahiki zao na pia wamiliki watakaojiunga na vyama vya ushirika au kuwa na makampuni watapunguza garama za uendeshaji kwa kuwa basi moja linauwezo wa kubeba abiria 90 sawa na mabasi madogo sita ya abiria”alisema Ngewe.
Naibu Mrajisi tume ya maendeleo ya ushirika Charles Malunde alisema kuna zaidi ya wanachama millioni 9 nchi nzima, na kuwasihi wamiliki wa gari za abiria wajiunge na vyama vya ushirika kwa maendeleo yao na Taifa.
Naye, Mwenyekiti wa chama cha madereva wa daladala kanda ya Ziwa Dede Petro alisema hatua hiyo itawasaidia wananchi kupunguza gharama ya usafiri kwa kuwa na huduma bora pamoja na ajira za kudumu kwa madereva na makondakta.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.