TAASISI ZOTE MWANZA ZATAKIWA KUJISAJILI PDPC
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amezitaka Taasisi zote za Umma na binafsi Mkoani humo kuhakikisha wanajisajili katika Mfumo wa Usajili na Uzingatiaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC )kabla ya Tarehe 30 Aprili, 2025 ambayo ni ukomo wa kujisajili kwa hiari baada ya muda wa nyongeza uliotolewa na Tume.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mhe. Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wakati wa kufunga Warsha maalumu kwa Kamati ua Usalama Mkoa pamoja na Wadau wa Taasisi za Umma na Binafai leo machi 28, 2025.
Mhe. Mtanda amesema baada ya tarehe hiyo ya ukomo taasisi zote zitakazoshindwa kujisajili zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni na sheria za kiutawala.
“Na nitumie nafasi hii kumuagiza Katibu Tawala Mkoa kuhakikisha barua hizo ulizoletewa kutoka Tume kuhakikisha zinazifikia Taasisi zote kwa utekelezaji”.
Aidha, ameziagiza pia Taasisi zote za Umma na Binafsi kuteua Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (DPOs) ambao watahusika moja kwa moja na usimamizi wa ulinzi wa taarifa binafsi ndani ya Taasisi zao kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa usalama wa taarifa binafsi ni msingi wa maendeleo ya kidigitali na uaminifu katika utoaji huduma nchini, hivyo ametoa rai kwa washiriki hao kutumia fursa hiyo kujifunza kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha mifumo ya ulinzi wa taarifa binafsi Mkoani Mwanza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PDPC Dkt. Emmanuel Mkilia amesema Mkoa wa Mwanza ni Mkoa unaokua kwa kasi na kuna umuhimu mkubwa wa utekekezaji wa sheria hiyo ambapo kwa sasa ni Taasisi 20 pekee ndio wamejisajili hali inayotakiwa kubadilika ili Mkoa pia utajwe kuwa mfano katika ulinzi wa taarifa binafsi
Aidha Tume hiyo imemuomba Mkuu wa Mkoa kuhamasisha Taasisi hizo kufanya warsha kwa watumishi wao ili kuongeza uelewa wa ulinzi wa taarifa binafsi na wajibu wa Taasisi katika kulinda utu na faragha za watu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.