Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala amesema Tanzania itakuwa moja ya taifa tajiri endapo itachukua hatua madhubuti ya kuhifadhi maliasili zilizopo kwa sasa.
Dk. Kigwangala amesema Tanzania ndani ya miaka 10 ijayo watanzania watakadiriwa kufikia milioni 100 na baada ya miaka 100 watafikia milioni 200, hivyo kutakuwa na changamoto kubwa ya mahitaji ya binadamu kama maji, umeme, ardhi, chakula na hewa.
Alisema endapo hatua za uhifadhi wa maliasili zitachukuliwa mapema, Tanzania itakuwa tajiri na taifa lenye usalama zaidi kutokana na kuwa na hifadhi za taifa, maziwa, mito na ardhi ya kutosha tofauti na mataifa mengine hivyo watanzania watakuwa na uwezo kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa misimu mitatu kwa mwaka.
“Tanzania ni moja ya nchi iliyo tofauti na mataifa mengine, imejaliwa na kuwa na maliasili na vivutio kadhaa ambavyo hata nchi nyingine hazitapata tulichonacho, naomba niwaambie hifadhi ni utajiri mkubwa sana.
“Nasema hivyo kwa sababu idadi ya watu inaongezeka kila siku tena kwa kasi kubwa lakini vile vitu tunavyohitaji ili tuishi ni vile vile na tusipovitunza kizazi kijacho cha watanzania wa miaka 50 ijayo kitakadirikiwa kufikia milioni 100, baada ya miaka 100 tena tutafikia milioni 200 hebu tujitafakari hapo mahitaji yatakuaje.
“Mahitaji yatakuwa makubwa kuazia maji, umeme, chakula , hewa na vitu vingine na kama Tanzania tutachukua hatua mapema ya kulinda rasilimali zilizopo tutakuwa na taifa tajiri kwa sababu tuna maji ya baridi tunayo ambayo pengine watanzania wanaweza kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji mara tatu kwa mwaka na kuachana na kutegemea mvua.
“Leo baadhi ya nchi za Afrika zimeanza kulalamika kukosa chakula na mmeona juzi juzi Mhe. Rais Dkt.John Magufuli ametembelea baadhi ya mataifa ikiwamo Zimbabwe wametuomba chakula na tumetoa, Tanzania tuna vitu vya kipeke kama hifadhi ya Serengeti ambayo nchi nyingine hazina, hivyo vitu kama hivi lazima tutunze, huwezi kuamini Ziwa Manyara linaweza kutoweka kutokana na kina chake kupungua, leo ukiambiwa Sinza au Magomeni pale Dar es Salaam kulikuwa na bwawa huwezi kuamini,”alisema.
Dk. Kigwagala alisema hapo mbeleni kutakuwa na shida ya maji sana na wabunge wa miaka 50 au 100 ijayo watakuwa wanadaiwa na wananchi wake kupelekewa huduma ya maji ya bomba kwa ajili ya kilimo na si matumizi ya nyumbani kama ilivyo sasa.
Tanzania kwa miaka hiyo itakuwa tajiri kutokana na kuwa na ardhi na maji ya baridi ambapo kuna uwezekano wa kuwa na maghala ya chakula kwa ajili ya kuzihudumia nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Aliongeza kuwa hivi sasa Serikali imekusudia kujenga kivuko cha watalii wa majini ambapo kitafanya shughhuli ya kutembelea hifadhi ya kisiwa cha Saanane, Chato, Lubondo na hifadhi zingine zilizo pembezoni mwa ziwa Viktoria.
Alisema sekta ya utalii ndio inaongoza kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia tano, hivyo ni dhahiri inapaswa kutunza kikamilifu.
Naye Kamishna wa Tanapa, Allan Kijazi alisema hifadhi za taifa zilizopo kaskazini ndio zinaongoza kutembelewa na watalii tofauti na kanda zingine ambapo kama Serikali imejapanga kufanya mageuzi ili hifadhi zingine ziweza kufahamika zaidi na kutembelewa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella alisema mkoa huo ni kitovu cha nchi za Afrika Mashariki na ndio njia ya karibu kwenda hifadhi ya Serengeti ambapo aliongeza kuwa kisiwa cha Saanane ambacho ni pekee kutokana na kuwa ndani ya Ziwa Viktoria na Jiji la Mwanza.
Hata hivyo aliziomba wizara nyingine kutembelea mikaoni na kutoa mikakati yao ili viongozi wa mikoa waweze kujua cha kufanya wakati wakitimiza wajibu wao.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wahariri wenzake, Abdallah Majura, alisema semina hiyo kwa wahariri na waandishi waandamizi itawaongezea maarifa mapya juu ya masuala ya Tanapa huku akimpongeza Dk. Kigwangala namna alivyoongoza wizara hiyo na kuleta mafanikio chanya kwa muda mfupi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.