Serikali imezitaka kampuni kutoka mataifa ya Kenya, Uganda, China, Egypt na India ambazo zimekuwa zikishiriki maonesho ya Afrika Mashariki yanayoandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara,wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na yale ya kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba kujenga viwanda vyao nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka ambaye alimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa katika ufunguzi wa maonyesho ya 14 ya TCCIA yanayofanyika katika viwanja vya jengo la biashara la kimataifa la Rocky City Mall, jijini Mwanza.
Rutageruka amesema sababu ya Serikali kuzitaka kampuni hizo kujenga viwanda vyao nchini kutokana na bidhaa zao zinakubalika kwa watanzania na zaidi katika kushindanisha washiriki wa maonyesho mbalimbali zimekuwa zikiibuka na ushindi wa jumla na kujizolea vikombe vingi.
Alisema hakuna haja ya kampuni hizo kuendelea kupata usumbufu wa kusafirisha bidhaa zao kila mwaka kuleta Tanzania kwa ajili ya maonyesho, hivyo ni wakati muafaka wa kuwekeza nchini kwa kujenga viwanda ikiwa ni sehemu ya uwekezaji kwani tayari soko limepetikana.
“Ninachozungumza hapa ni cha waziri Bashungwa ambaye anasema wakati Serikali inawakaribisha wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza nchini kutokana na bidhaa zao kukubalika, ni wakati muafaka kwa watanzania kujifunza na kuiga kile kinachofanywa na wenzetu, tusiendelee kupenda vya wengine na kusahabu vya kwetu.
“Mimi ni mzoefu katika maonyesho haya ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka, ukifika katika mabanda ya washiriki wakigeni unakuta watanzania wamefurika pale wakinunua bidhaa zao, mfano kampuni ya Movit ya Uganda inakuwa na wateja wengi, sasa hakuna haja kila mwaka kusafirisha bidhaa, kama Serikali tunawataka waje tuwape maeneo ya kujenga viwanda vyao.
“Tanzania ni salama na inawakaribisha wawekezaji kutoka Kenya, Uganda, China, Egypt na India kwani hawa kila mwaka wanapata vikombe vya washiriki na bidhaa bora, hata leo sote tumeshuhudia hapa zawadi nyingi zimechukuliwa na kampuni za nje, naomba viwanda vijengwe hapa Mwanza kwani ndio kitovu cha nchi za Afrika Mashariki,”alisema.
Katika hatua nyingine, Rutageruka alisema sekta ya kilimo inaendelea kukosa mvuto kwa watanzania na wengi wao wamegeukia biashara ambapo aliwashauri viongozi TCCIA wanaoshughulikia sekta ya kilimo kuendelea kuhamasisha wananchi kuachana na kilimo cha jembe la mkono na kulima kisasa.
Wakati huo huo,alisema asilimia 70 ya wafanyabiashara wa mipakani ni wanawake ambao wengi wao wanafanya shughuli za kiuchumi zisizo rasmi hivyo aliwataka viongozi wa TCCIA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuwalimisha ili kutambulika.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Dkt. Elibariki Mmari alisema changamoto iliyopo kubwa ni washiriki kutoka nje ya Tanzania kusumbuliwa mipakani wanapotaka kuingiza bidhaa zao kwa ajili ya maonyesho hayo kwani huchukua muda mwingi kuthibitisha bidhaa.
Dkt. Mmari aliendelea kuiomba Serikali kuwapatia eneo la Nyamhongolo jijini Mwanza ambalo limekuwa likitumika katika maonyesho ya wakulima maarufu nane nane ili kuliwekeza katika hadhi ya kimataifa.
Dkt. Mmari alisema miongoni mwa fursa zitakazopatikana kutokana na maonyesho hayo ni kuimarisha mtandao wa masoko na usambazaji bidhaa, kampuni za Tanzania kujifunza na kutanua wigo wa biashara kwa kutumia makubaliano ya kibiashara ya kimataifa.
Vile vile alisema kufanyika maonyesho hayo yanatoa mchango kwa vitendo katika kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. John Magufuli kuifanya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikipo 2025 sambamba na kuimarisha mtengamano wa soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.