Wamiliki wa magari na madeva jijini Mwanza waliozoea ‘kumalizana’ na wakata ushuru wa maegesho itabidi sasa hawatakuwa na njia zaidi ya kulipa ushuru halali baada ya shughuli hiyo kukabidhiwa kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).
Baada ya kukabidhiwa kazi hiyo ambayo awali ilifanywa kwa uwakala kati ya kampuni binafsi na halmashauri, Tarura imetangaza kuanzisha mfumo wa kielektroniki utakaolipiwa moja kwa moja kwa njia ya mtandao.
Akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa barabara jijini Mwanza leo Julai 20, Mratibu Tarura Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Koyoya Fuko amesema mfumo huo utaanza kufanya kazi miezi mitatu kuanzia sasa.
“Kwa kushirikiana na Kampuni ya NPK Technology ya jijini Dar es Salaam, Tarura itafunga vifaa za kisasa zikiwemo kamera za CCTV katika mitaa yote ya jiji la Mwanza zitakazonasa na kuratibu shughuli za maegesho na malipo,” amesema Mhandisi Fuko.
Pamoja na malipo ya maegesho, kamera hizo pia zitasaidia masuala ya ulinzi na usalama mitaani kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi mienendo inayotiliwa mashaka yanapobainika mitaani.
“Mapato ya ushuru wa maegesho unatarajiwa kupanda kutoka Sh500 milioni za sasa hadi kufikia Sh2.5 bilioni kwa mwaka,” amesema Fuko.
Mfumo huo unaofanyiwa majaribio jijini Mwanza kabla ya kuenezwa nchi nzima pia utasaidia kuimarisha usafi mitaani kwa kubaini maeneo ambayo uchafuz umerundikana na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Licha ya kuonyesha masikito kwa sehemu ya mapato ya halmashauri kutwaliwa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga amesifia mfumo huo kuhusu upande wa suala la usafi mitaani akisema utasaidia kuyabaini na kutoa taarifa ya maeneo yenye mirundikano ya takataka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.