CHEMBA ya Wafanyabiashara,wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) imeiomba Serikali kuipatia eneo la Nyamhongolo jijini Mwanza ambalo limekuwa likitumika katika maonyesho ya wakulima maarufu nane nane ili kuliwekeza katika hadhi ya kimataifa.
Ombi hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Dkt. Elibariki Mmari wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ufunguzi wa maonyesho ya 14 ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kuzinduliwa Agosti 30, mwaka huu na Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Innocebt Bashungwa.
Dkt. Mmari amesema maonyesho hayo yanafanyika katika viwanja vya jengo la Biashara la Kimataifa la Rocky City Mall jijini Mwanza ambapo nchi za Kenya, Uganda,Rwanda, Indonesia, India, Syria, China na kampuni 300 zimethibitisha kushiriki.
Ameongeza kuwa TCCIA imekuwa katika changamoto ya muda mrefu ya kupata eneo la kudumu la uwekezaji kwa ajili ya maonyesho hayo ambapo ilifanya mazungumzo ya awali na uongozi wa Mkoa wa Mwanza lakini walishindwa kufikia muafaka kuwapo na mpango wa maonyesho ya nanenane kikanda.
“Kama Serikali itatupatia pale Nyamhongolo tuna uwezo wa kujenga majengo yenye hadhi ya kimataifa na shughuli zitakuwa zikifanyika kwa mwaka mzima badala ya kusuburia nanenane, tutakachofanya ni kuzingatia mahitaji makundi yote ambapo wale watakaokuwa wanahitaji eneo ni kulipia kama kawaida.
“Awali tulifanya mazungumzo na viongozi wa mkoa lakini kukawa na taarifa ya maonyesho ya nanenane yanatakiwa kuhamia Mwanza ambapo mpango huo ulishindikana na kuwapo mgawanyo, sote ni mashahidi wengine wanafanyia Simiyu, mikoa mingine hapa Mwanza.
“Bado tunafuatilia suala hili lakini tunaiomba Serikali itupatie lile eneo ili tulifanyie uwekezaji mkubwa na kuwa na hadhi ya kimataifa ili mataifa yanayohudhuria maeonyesho yetu yawe na uhalisia wa kile tunachokifanya, kwanza mapato ya nchi yatapatikana kwa urahisi na shughuli zitakuwa zikifanyika muda wote wa mwaka kama ilivyo Rocky City Mall,”alisema.
Dkt. Mmari alisema maonyesho ya mwaka huu yatakuwa tofauti na miaka mingine kutokana na mataifa makubwa nje ya Afrika Mashariki kushiriki ambapo mapungufu yote yaliyojitokeza mwaka jana yamefanyiwa kazi huku akiwataka wananchi kujitokeza kutembelea kwani kutakuwapo na wanyama wakiwamo simba, fisi,chui, ngamia na wengine ambao watapata fursa ya kuwaona na kupiga picha.
Dkt. Mmari alisema miongoni mwa fursa zitakazopatikana kutokana na maonyesho hayo ni kuimarisha mtandao wa masoko na usambazaji bidhaa, kampuni za Tanzania kujifunza na kutanua wigo wa biashara kwa kutumia makubaliano ya kibiashara ya kimataifa.
Vile vile alisema kufanyika maonyesho hayo yanatoa mchango kwa vitendo katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli kuifanya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikipo 2025 sambamba na kuimarisha mtengamano wa soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Hata hivyo alipiga marufuku baadhi ya bidhaa zikiwamo silaha za moto na milipuko, masuala ya siasa na dini hayaruhusiwi katika maonyesho hayo huku akiwataka kampuni na watu binafsi wanaotaka kuwa wadhamini katika shughuli hiyo kujitokeza kabla ya Agosti 25, mwaka huu.
Alisema maonyesho hayo yatakuwa na zawadi kwa washindi katika makundi mbalimbali yakiwamo wahandisi, kilimo, viwanda, chakula, dawa na makundi maalum ambapo aliwataka washiriki kutambua jopo la majaji litaanza kupita kwenye mabanda yao kuanzia Agosti 31 hadi Septemba Mosi mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.