MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imefanya ziara ya kushtukiza katika kampuni tano za mawasiliano kwa lengo la kuona namna ya zoezi la usajili wa laini kwa kutumia mfumo wa alama za vidole(Biometric) linavyofanyika huku wananchi wakifurahia jinsi wanavyohudumiwa licha ya kuwapo na msongamano mkubwa.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo na watumishi wenzake watano pamoja na waandishi wa habari huku wakitembea kwa miguu, walianzia ukaguzi kampuni ya Halotel na kukagua mashine za usajili zinavyofanya kazi na kuwahoji wananchi wanaosajiliwa.
Pia walikwenda kampuni ya Airtel, Vodacom, Tigo, Smile na TTCL ambapo licha ya kuwapo na kasoro ndogo ndogo za kimtandao, zoezi hilo lilionekana kuwafurahisha wananchi baada ya Mhandisi Mihayo kutoa maelekezo kwamba wananachi wote wenye vitambulisho tofauti na vile kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) nao wasajiliwe na kuwapa elimu kwamba usajili huo ni wa muda ambapo unakoma Desemba mwaka huu.
Changamoto ndogo zilioonekana kutoka kwenye baadhi ya kampuni zilizotembelewa ni mashine zinazochukua alama za vidole kutokuwa na mawasiliano ya kutosha kati yao na NIDA kitendo ambacho kinasababisha wananchi kukaa muda mrefu kwenye foleni.
Vile vile baadhi ya vyumba wanapofanyia usajili huo kuzidiwa na watu ambapo wengine hulazimika kupanga foleni nje ambapo Mhandisi Mihayo ameelekeza kila kampuni kuongeza mashine ili kurahisisha zoezi hilo na pale wanapohitaji msaada wowote wasisite kufika TCRA.
Hata hivyo wananchi wengi waliomba kampuni kuweka utaratibu wa kuwahudumia wazee na akina mama wenye watoto na wajawazito ili kuepuka kukaa muda mrefu kwenye foleni, pia waliomba usajili huo ufanyike maeneo mablimbali kuepusha gharama za kusafiri kwenda mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Mhandisi Mihayo, alisema lengo ni kusimamia utekelezaji wa usajili wa laini kwa mfumo wa biometric na kuona linavyofanyika na changamoto zake ingawa tathimini ya haraka tunaweza kusema zoezi linakwenda vizuri sana.
“Kikubwa tulichokuiona ni mwitiko kuwa mkubwa na kusababisha foleni, sasa hapa nilipo nafikiria siku ya kuwaita viongozi wa kampuni hizo kwa kanda ya ziwa ili waje hapa tupange namna ya kuongeza vituo vya usajili, tumeshuhudia pale Airtel na voda watu walivyokuwa wengi.
“Rai yangu kubwa kwa watanzania tusisubiri zoezi hili mpaka ifike Desemba ndio tujitokeze kwenda vituoni, tutakuwa tumechelewa naomba wananchi pale anapopata nafasi akasajili laini yake, wenye vitambulisho vya NIDA wao watapata usajili wa kudumu na si lazima uende na kitambulisho hata namba zenyewe zinatosha.
“Wale wenye vitambulisho vingine kama leseni ya udereva, kadi ya mpiga kura na vingine vilivyoruhusiwa hao watasajiliwa kwa usajili wa muda hadi Desemba, baada ya hapo namba usajili huo utafutwa, leo nimefanya ziara hii mjini lakini najipanga kwenda vijijini katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa,”alisema.
Naye Meneja Huduma kwa Wateja Kanda ya Ziwa kutoka Kampuni ya Tigo, Beatrice Kinabo alisema mpaka sasa wana maduka mawili jiji la Mwanza ya usajili na huku Ukerewe likiwapo moja ambapo kwa siku wanasajili zaidi ya wateja 100.
Kinabo alisema kwa Mkoa wa Mwanza wana mashine zaidi ya saba zinazotumika kusajili wateja wao ambapo nguvu sasa ipo katikati ya Jiji la Mwanza na baadaye watakwenda wilayani.
Kwa upande wa Mtendaji Kiongozi wa Kanda ya Ziwa kutoka Vodacom, Dominishan Mkama alisema kwa siku ya juzi walisajili wateja 250 lakini jana mashine ilionekana kuwa na kasoro wakati wakiendelea na zoezi hilo ambapo alifafanua kwamba tayari amewasiliana na NIDA na kuahidiwa kulitatua haraka.
Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Mwanza, Jalili Bakari alisema zoezi hilo linakwenda vizuri ingawa changamoto ndogo ndogo za kimtandao zinasumbuaa ambapo kwa siku wanasajili watu 100 na kuendelea, hivyo aliomba NIDA kushirikiana pale inapotokea tatizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.