Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaonya washiriki wa maonyesho ya 14 ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kuzinduliwa Agosti 30, mwaka huu mkoani Mwanza, kwamba atakayekiuka sheria na taratibu atakumbana na adhabu ya kifungo au faini inayofikia Sh milioni nne.
Onyo hilo limekuwa ikiwa ni siku moja baada ya Chemba ya Wafanyabiashara,wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kutangaza siku ya ufunguzi wa maonyesho ya 14 ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kuzinduliwa Agosti 30 na kufikia tamati Septemba 8, mwaka huu huku mataifa nane na kampuni 300 kuthibitisha kushiriki.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Joseph Mtandika alisema wamejipanga kuhakikisha kila mshiriki wa maonyesho hayo anazingatia sheria na taratibu zilizopo zikiwa za kutoa na kudai stakabadhi ya mashine ya elekitroniki ( EFD) iliyo na gharama halilsi ya kile alichokinunua au kuuza.
Mtandika alisema sheria zinamtaka mtu yeyote ambaye mauzo yake kwa mwaka yanafikia Sh milioni 14 na kwa siku Sh 39,000 anapaswa kuwa na mashine ya EFD ambapo aliainisha kwamba atakayenunua kitu bila kudai stakabadhi adhabu yake ni kifungo au kulipa faini inayoanzia Sh 30,000 hadi Sh milioni 1.5.
“Adhabu kwa muuzaji ambaye atashindwa kutoa stakabadhi kwa mteja wake, akikamatwa atalazimika kulipakati ya Sh milioni tatu hadi nne kulingana na uzito wa kosa unaoendana na kile alichokiuza, tunaomba wafanyabiasha waache visingizio juu ya suala la kodi.
“Kama mashine ya EFD imekuharibikia ukiwa katika maoenyesho hayo unatakiwa kutoa taarifa TRA na yule aliyekuuzia hiyo mashine, pia vile vitu ambavyo ataendelea kuviuza wakati akisubiria mashine ile kutengenezwa ni lazima atoe stakabadhi ya kitabu cha mkono ambapo sisi kama TRA tutapita kukagua ili kujiridhisha.
“Baada ya mashine kurejeshwa anatakiwa taarifa zote zilizopo kwenye stakabadhi ya kitabu cha mkono aziingize kwenye mashine ili kuweka kumbukumbu sawa, kama TRA tutashiriki na tutatembelea washiriki wote na kuwapa elimu, pia kwa wale ambao watakuwa na uwezo wa kuingia kwenye tovuti zetu watapata kila kitu,”alisema.
Mtandika alisema waonyeshaji au wauzaji wa bidhaa wanatakiwa kuwasilianana TRA au mawakala wa kusafirisha mizigo (clearing and fowaring arget) ili kupata taarifa na a taratibu za kuingiza mizigo kutoka nje ya nchi zikiwamo ushuru wa forodha, ushuru wa bidhaa.
Hata hivyo meneja huyo aliwaomba viongozi wa TCCIA kuwaelimisha washiriki wa maonyesho hayo ili Serikali isiweze kupoteza mapato.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Dk. Elibariki Mmari, alisema bidhaa zitakazoonyeshwa katika maonyesho hayo ni kundi la vyakula, kilimo na vinywaji, nguo, ngozi, vifaa vya viwandani, ujenzi, umeme, pembejeo za kilimo, urembo, mbao za samani, uhandisi na huduma za kibiashara.
Alisema maonyesho hayo yatafanyika katika viwanja vya jengo la Biashara la Kimataifa la Ricky City Mall jijini Mwanza ambapo nchi za Kenya, Uganda,Rwanda, Indonesia, India, Syria, China na kampuni 300 zimethibitisha kushiriki ambapo yatafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa Agosti 30 na kufunga Septemba 8, mwaka huu.
Dk. Mmari alisema miongoni mwa fursa zitakazopatikana kutokana na maonyesho hayo ni kuimarisha mtandao wa masoko na usambazaji bidhaa, kampuni za Tanzania kujifunza na kutanua wigo wa biashara kwa kutumia makubaliano ya kibiashara ya kimataifa.
Vile vile alisema kufanyika maonyesho hayo yanatoa mchango kwa vitendo katika kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli kuifanya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikipo 2025 sambamba na kuimarisha mtengamano wa soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.