Tuhakikishe Maafisa Utumishi Wanatekeleza Majukumu yao bila Kikwazo: Waziri Simbachawene*
Waziri wa Nchi, Ofis ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Mhe. George Simbachawene amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanawajengea uwezo Maafisa utumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Waziri Simbachawene ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 03, Agosti 2023 wakati akizungumza na watumishi kwenye mapokezi yake alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya ziara ya kikazi ya Siku mbili.
Amesema, katika uboreshaji wa sekta za utumishi na Rasilimali watu idara hiyo ina majukumu mazito kama ufuatiliaji wa nidhamu, kupandishwa vyeo na uhuishaji wa taarifa za kiutumishi kwenye mfumo ambapo kwa pamoja zinahitaji umakini na weledi.
"Tuhakikishe Maafisa utumishi wanatekeleza Majukumu yao bila kikwazo ili waweze kuwa na utulivu wa utendaji kazi wenye weledi wakati wote katika kukuza sekta hii muhimu." Amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Vilevile, Mhe. Waziri amewaagiza Maafisa utumishi kuhakikisha kujaza taarifa za watumishi kwenye mfumo wa utumishi ili kurahisisha utendaji kama upandishaji wa madaraja na uwajibishaji wa masuala mbalimbali ya kinidhamu.
Akimkaribisha Mhe. Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amempongeza kwa utendaji wake mahiri unaodhihirisha dhamira ya Serikali katika kuboresha sekta ya Utumishi na utawala bora nchini na amemuahidi ushirikino katika kipindi chote cha ziara yake mkoani humo.
"Mhe. Waziri sisi tunakushukuru sana kwa kutupa upendeleo maana Mkoa wa Mwanza umekua Mkoa wako wa kwanza kufanya ziara ya kiutumishi na ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na wizara yako maana yake sasa upo 'Site'." CPA Makalla.
Waziri Simbachawene yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na masuala ya kiutumishi anatarajiwa kukagua miradi inayotekelezwa na Mfuko wa kunusuru kaya masikini -TASAF katika wilaya za Kwimba na Misungwi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.