Tulilinde Ziwa Victoria ili litupe Matunda : Byabato
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Afrika
Mashariki) Mhe. Steven Byabato leo Septemba 26, 2023 amefika Kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kufuatia ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya kisekta mkoani humo.
Akiongoza ujumbe alioongozana nao kwenye mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Byabato ametoa wito kwa wadau kwenye ukanda huo kulilinda Ziwa Victoria kwa maslahi ya vizazi vya sasa na baadae.
Amesema ziwa hilo linalounganisha Mataifa mbalimbali Afrika kwa dahari ya miaka limekua likistawisha uchumi wa Utalii na ukuaji wa sekta ya uvuvi hususani kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo kila mmoja anapaswa kulilinda lisiharibiwe wala kuchafuliwa.
Tunalilinda ziwa letu ili nalo litulinde sisi, sheria za usimamizi wa bonde la ziwa Victoria ni lazima zizingatiwe ili ziwa letu lilete matunda kwetu sio tu kwa usafirishaji na chakula bali hata kwa uchumi wa uvuvi na Utalii." Amesema Byabato.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati Mkoani humo huku akitolea mfano wa Daraja la Kigongo Busisi, Meli ya MV Mwanza, Machinjio ya Kisasa, miradi ya usafi wa mazingira pamoja na mradi wa Maji wa Butimba ambao uko mbioni kukamilika.
Mhe. Makilagi amefafanua kuwa miradi hiyo ni kielelezo kwamba Mhe. Rais Samia amekusudia kuwahudumia wananchi kwa kuwaondolea kero kwenye huduma za kijamii kwenye sekta za Miundombinu, Maji, Afya, Kilimo, Usafi wa Mazingira na Elimu.
Ziara ya Mhe. Byabato Mkoani Mwanza imejikita kwenye ukaguzi wa miradi mbalimbali ukiwemo Mradi wa Usafi wa Mazingira Pasiasi unaosimamiwa na Bonde la ziwa Victoria ambapo atajionea hatua ya utekelezaji iliyofikiwa kwenye miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.