TULINDENI NGUVU KAZI YA TAIFA KWA KUWACHANGIA FEDHA WATOTO WENYE SARATANI: RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda leo Mei 4, 2024 amezindua rasmi mbio za Bugando Health Marathon zenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu kwa watoto wenye Saratani na wasio na uwezo wa kumudu matibabu hayo.
Akizungumza na washiriki wa mbio hizo kwenye Hospitali ya Bugando, Mtanda amezitaka Taasisi na wananchi wote watakaojaaliwa kuunga mkono zoezi hilo ili kulinda nguvu kazi ya Taifa.
"Awali ya yote niupongeze uongozi wa Hospitali ya Bugando chini ya Mkurugenzi wake Dkt. Fabian Masaga, kwa ubunifu huu wa kutafuta fedha kwa nia njema ya kuokoa vizazi vyetu,ni ukweli gharama ya matibabu ya Saratani ipo juu na wengi hatuwezi kuimudu," Mhe.Mtanda.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyeshiriki mbio za km 5 amesema mpango huo umekuja wakati mwafaka hasa kutokana na idadi ya watoto wanaogundulika na Saratani kuongezeka kutoka 50 kwa mwaka hadi 300, hivyo jitihada kama hizo zinapaswa kuungwa mkono.
"Nimeguswa na zoezi hili la uchangiaji na Ofisi yangu inatoa shs milioni 5 nikiwa na imani wengi mtajitokeza ili kufaniikisha malengo ya kuwasaidia watoto hawa,"amesisitiza Mhe.Mtanda
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Dkt.Fabian Masaga amebainisha malengo ya mbio hizo za Marathon ni kupata zaidi ya shs bilioni moja zitakazowasaidia watoto wasio na uwezo,malengo mengine ni kuhamasisha jamii kujenga tabia ya kuchangia,kuhimiza kushiriki michezo na kufahamiana kwa ujumla.
"Ada ya ushiriki wa mbio hizi ni shs 35,000 na tutakuwa tukifanya mazoezi haya kila Jumanne na Ijumaa kabla ya kilele chake Agosti mwaka huu ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko atakuwa mgeni rasmi,"Dkt.Masaga
"Ugonjwa huu unatibika endapo mtoto ataletwa mapema Hospitali,changamoto ipo kwa baadhi ya wazazi kuanza kukimbilia tiba mbadala na baadaye kuja Hospitali wakati tayari ugonjwa umepiga hatua kubwa,"Dkt.Yoronimo Kashaigili,bingwa wa ugonjwa wa Saratani kwa watoto.
Kauli mbiu ya mbio za Bugando Health Marathon inasema,Kimbia,changia watoto wenye Saratani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.