TULITUMIE JUKWAA LA UMISSETA NA UMITASHUMTA KUPATA HAZINA YA WANAMICHEZO WA TAIFA:RAS BALANDYA
Mashindano ya Michezo ya Umoja wa Shule za Sekondari UMISSETA na Umoja wa Shule za Msingi UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa wa Mwanza yamefungwa leo rasmi na rai kutolewa Jukwaa hilo litumike vizuri kupata hazina ya wanamichezo wa Taifa.
Akifunga mashindano hayo leo Alasiri kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Nsumba kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Bw.Daniel Machunda amesema wanamichezo nyota wanaotamba hivi sasa Duniani wameanzia ngazi kama hizi na kupata muendelezo mzuri,hivyo hatuna budi kuvibaini vipaji vinavyoonekana na kuviwekea mkakati maalum wa kuviendeleza.
"Kwa muda mfupi nimekaa hapa nimeona uwezo mzuri wa vijana wetu hasa katika sanaa za ngoma na kwaya,ni jambo la kujivunia sana,hii ni hazina nzuri ya Taifa tunaishukuru Serikali kwa kuweka mashindano haya kila mwaka"amesisitiza Machunda.
Aidha amewataka wanamichezo wote bora waliopata nafasi ya uteuzi kwenda kushiriki mashindano ngazi ya Taifa kutanguliza nidhamu ambayo ndiyo silaha ya mafanikio.
"Sasa hivi wanamichezo ndiyo wanalipwa fedha nyingi Duniani,lakini hadi kufikia hatua hiyo nidhamu ndiyo silaha ya pekee ni lazima mjitambue,muwe wasikivu kwa walimu wenu,ongezeni bidii na kuzingatia maelekezo yote ya msingi huo ndiyo msingi wa kupata mafanikio,"Machunda
Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi Afisa Michezo Mkoa wa Mwanza,James William amebainisha mashindano hayo yameshirikisha michezo 9 ukiwemo soka kwa wavulana na wasichana,mpira wa kengele kwa albino na wenye ulemavu wa macho,mpira wa kikapu,pete,mezani,wavu na mikono kwa wasichana na wavulana pia imeshirikishwa sanaa za jukwaani ambazo ni kwaya,ngoma,mziki wa kizazi kipya(Singeli) na uchekeshaji.
"Ndugu mgeni rasmi tumepata jumla ya wanamichezo bora 120 na tumeongeza 40 tutafanya mchujo ili kuwapata 120 watakaokwenda kushiriki ngazi ya Taifa huko mkoani Tabora kuanzia Juni 17 hadi 27 mwaka huu",Afisa Michezo.
Katika mashindano ya ngazi ya Mkoa mwaka huu mshindi wa jumla ni Wilaya ya Nyamagana ikufuatiwa na jirani zao Ilemela.
Kwa miaka minne mfululizo Mkoa wa Mwanza umeshika nafasi ya pili Kitaifa kwenye Mashindano ya Umissseta
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.