Tumieni Mafunzo ya Kizazi chenye Usawa kuleta Tija kwa Taifa: RAS Balandya
Leo Januari 16, 2024 Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amefunga rasmi mafunzo ya kizazi chenye usawa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Mikoa 15 na kuwataka kulitumia vyema jukwaa la mafunzo hayo ili yawe na tija kwa Taifa.
Akizungumza na washiriki hao kuanzia ngazi ya mkoa, halmashauri na kata kwenye ukumbi wa halmashauri ya Jiji, Balandya amesema uzingatia wa masuala ya jinsia ni mojawapo ya nguzo muhimu ili kufikia maendeleo jumuishi na endelevu kiuchumi,kijamii,kisasa na kiutamaduni.
Amesema Serikali kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo imewashirikisha ili kwenda kuleta mageuzi chanya ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake hapa nchini.
"Ndugu washiriki mkumbuke mkutano wa kimataifa wa Beijing mwaka 1995 nchi yetu ilichagua kutekeleza maeneo 5 kati ya 12 ambayo ni uwezeshaji wanawake kiuchumi, kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi,elimu,ajira na mafunzo pamoja na kuingiza masuala ya jinsia katika sera, na bajeti za kisekta,"Katibu Tawala mkoa.
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi Idara ya jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,jinsia,wanawake na makundi maalum Juliana Kibonde amesema kipindi cha mafunzo hayo ya siku mbili washiriki wamefundishwa namna ya kubuni na kuandaa mikakati mbalimbali ya kiutekelezaji kwenye maeneo yao ya kazi ikiwemo mkakati wa mawasiliano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.