TUTUMIE MATAMASHA KUUTANGAZA UTAMADUNI WETU - DKT. BITEKO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dotto Biteko ametoa rai kwa Watanzania kutumia matamasha makubwa kama la Bulabo (Tamasha la sherehe za mavuno) kutangaza mila na tamaduni za Mtanzania, ikiwa ni njia muhimu ya utambulisho wa Taifa la Tanzania kimataifa.
Mhe. Biteko ametoa rai hiyo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Chifu Mkuu wa Machifu wote Tanzania (Chifu Hangaya) katika kilele cha Tamasha la Utamaduni la Bulabo Kanda ya Ziwa lililofanyika leo Juni 27, 2024 Bujora - Kisesa Wilayani Magu Mkoani Mwanza.
Mhe.Biteko amesema Taifa la Tanzania lina mila na tamaduni zake ambazo hurithishwa vizazi kwa vizazi ambapo ni lazima zilindwe na zihifadhiwe vizuri na kujiepusha na kupokea tamaduni za kigeni ambazo sio asili yetu.
"Ni lazima tulinde na kudumisha tamaduni zetu, Taifa lisilodumisha tamaduni zake, hilo ni Taifa la mazombi, hivyo ninawaasa tudumishe misingi ya mila, desturi na tamaduni zetu". Amesema Mhe. Dkt. Biteko.
Aidha Dkt. Biteko ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa Mkoa Mtanda kwa maandalizi mazuri na ya kiwango ya tamasha hilo la bulabo na kuahidi kwenda kuyasimulia hayo kwa Mh. Rais Samia, sambamba na hayo pia ametoa maagizo kwa Mikoa yote ya kanda ya ziwa kuhakikisha wanashirikiana vizuri katika kuandaa tamasha hilo kwa mwaka ujao ili kulifanya kuwa la viwango.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema wamedhamiria kulikuza na kuliendeleza tamasha hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo na kulitangaza pia kimataifa ili nalo lifanywe kuwa ni kivutuo cha utalii kwa kanda ya ziwa.
"Nina hakika mwakani tamasha hili litakua bora zaidi na niwahakikishieni kuwa tutatarajia kupokea zaidi ya watalii 100 kutoka nchini Brazili watakaokuja kushiriki katika tamasha la bulabo, lengo ni kuutangaza utamaduni wa kabila la kisukuma kimataifa".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.