Serikali imevutiwa na uchapakazi wa vijana wilayani Ukerewe ikisema jambo ni tofauti na wilaya nyingine kwa sababu vijana wengi hawataki kuwekeza kwenye kilimo na hata waliowezeshwa kuanzisha miradi ya maendeleo, mingi imekufa kwa kukosa matunzo.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Omari Mgumba wakati akizungumza na kikundi cha vijana wa Kata ya Bugorola wilayani humo baada ya kuonyesha kuridhishwa na kuvutiwa na mradi wa umwagiliaji wa kikundi hicho cha vijana na kwamba hakuna mtu kutoka nje atawaletea maendeleo.
Alisema vijana wengi hawako tayari kuwekeza kwenye kilimo badala yake wamekuwa wakikimbilia mijini na kuwaacha wazee vijijini wakiendesha kilimo, tofauti na Wilaya ya Ukerewe ambako vijana wanajituma na kuchapa kazi kwa kulima mazao mbalimbali na kufanya shughuli za uvuvi na ufugaji.
Mgumba alisema malengo ya Serikali ni kuona wananchi wanalima kwa tija ili kuongeza vipato vyao na kuinuka kiuchumi kupitia sekta ya kilimo, hivyo vijana ambao ni nguvu ya taifa watumie fursa hiyo na kuyatumia mabonde yaliyopo wilayani humo kwa kilimo chenye tija.
“Nimevutiwa na jinsi mnavyomuunga mkono Mhe.Rais John Magufuli na serikali yake kupitia kauli mbiu yake ya "Hapa Kazi Tu".Vijana wanawaacha wazee na kuhamia mijini lakini hapa Ukerewe vijana mnachapa kazi , mnalima pilipili hoho, mahindi,nyanya na mazao mengine .Mnajituma katika kilimo mazao, mifugo, uvuvi na misitu na kutunza mazingira na kuwawezesha kupata kipato na kuinuka kiuchumi,”alisema.
Akizungumzia chanzo cha maji cha mradi wa umwagiliaji wa Bugorola Naibu Waziri huyo wa Kilimo alisema una mchango mkubwa wa maendeleo kwenye sekta ya kilimo lakini kwa sasa ni chakavu kutokana na miundombinu yake kuwa ya muda mrefu na haukidhi tena mahitaji.
“Mradi huu kwa mujibu wa sheria umechakaa sana kwa sababu ni wa muda mrefu tangu ujengwe mwaka 1974, kuukarabati ni gharama kubwa pia mahitaji makubwa yameongezeka ambapo umekufa kwa kukosa matunzo kwani inahitaji kutunzwa ili iwatunze lakini ikifa itaonekana hamna nia serikali iwasaidie, hivyo wataalamu watakuja kufanya tathmini ya mahitaji ili fedha za kuuboresha ziletwe,”alisema Mgumba.
Aliongeza kuwa kazi ya serikali ni kuwajengea uwezo, haina fedha za matunzo na matengenezo ya mundombinu ya ya miradi ya umwagiliaji na kuwataka vijana 21 kati ya 100 wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji Bugorola kuonyesha mfano kwa wengine kwa kuchapa kazi ambapo serikali itawaunganisha na masoko ya uhakika wa mazao yao.
Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kufanya mapinduzi kwenye sekta ya kilimo ili wakulima walime kibiashara badala ya kilimo cha kujikimu ambapo imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa ajili ya kuwakopesha wakulima mitaji na matrekta.
Awali Ofisa Umwagiliaji wa Wilaya ya Ukerewe, Emil Sirwamba alimweleza Mhe. Mgumba kuwa kina cha maji cha mradi wa Bugorola kiko mbali na mfumo wake unatakiwa kubadilishwa ambapo eneo linalotumika kwa kilimo kwa sasa ni hekta 74 tu kati ya hekta 200 na kuiomba serikali iongeze fedha au ijenge chanzo na mfumo mpya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mradi wa Vijana Bugorola,Nicolaus Kusanya alisema kikundi hicho kiliundwa na vijana 100 lakini wamebaki 21 na kwamba wanakabiliwa na changamoto ya nishati ya mafuta kwa ajili ya kuvuta maji kutoka ziwani na kujaza kwenye tenki.
Diwani wa Kata hiyo Domician Mnyoro alisema changamoto kubwa ya kundi hilo la vijana wanaohangaika na kilimo ni ukosefu wa mitaji na pembejeo hivyo serikali iwasaidie na isisite kuwapa fursa zingine zinapopatikana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.