UJENZI DARAJA LA KIGONGO-BUSISI WAFIKIA 88.2%, RC MTANDA ASEMA HAKUNA KILICHOSIMAMA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la JPM (Kigongo-Busisi) lenye urefu wa KM 3.2 linalojengwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya zaidi ya Tshs. Bilioni 716.
Mtanda amesema chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Mwanza, ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 88.2 na akatumia wasaa huo kuwapongeza kwa kazi nzuri na akatoa wito kuendelea kusimamia ili ukamilike kwa wakati ifikapo Disemba 30 mwaka huu.
Mtanda ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kujenga daraja hilo kwa kasi kwani Rais Samia amelikuta likiwa chini ya asilimia 40 kiujenzi na hata malipo ya fedha lakini ndani ya miaka mitatu limeendelezwa bila kusimama na kwamba sasa wananchi wataondolewa adha ya msongamano kwenye vivuko.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatoa fursa kwa mikoa ya Kanda ya ziwa na nchi za jirani kuwa na hakika wa kufika kwa urahisi vilevile utasaidia kupunguza msongamano w magari kwenye vivuko vinavyotumika sasa na kwamba utarahisisha suala la usafiri kwa ujumla.
Mwakilishi wa Meneja wa TANROAD Mkoa huo Mhandisi Richard Ruyango amesema awali ujenzi wa daraja hilo ulioanza mwaka 2020 ulitarajiwa kukamilika Februari mwaka huu lakini kutokana na sababu mbalimbali mkandarasi huyo aliongezewa muda.
"Hatujaona mpango wa kujenga mzani upande wa Sengerema hivyo tunaomba ujengwe ili kulinda daraja letu maana uwekezaji huu ni lazima ulindwe kwa kuweka ukomo wa uzito wa magari kupita ili lidumu muda mrefu." Mhe. Hamis Tabasam, Mbunge wa Sengerema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.