UONGOZI MKOA WA MWANZA WAKARIBISHA WAWEKEZAJI FURSA ZA KIUCHUMI
Uongozi Mkoa wa Mwanza umeikaribisha kampuni ya Henan Afro-Asia Geo-Engineering Ltd ya China kuwekeza kutokana na fursa lukuki za kiuchumi mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Uongozi huo leo Machi 02, 2024 kwenye Hotel ya Malaika na uongozi na kampuni hiyo Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu, Daniel Machunda amesema Mkoa huo kuwa eneo la nchi za Maziwa Makuu, uimara wa njia kuu za usafirishaji, Utalii na hali ya hewa ya ustawishaji misitu ni miongoni mwa fursa za uwekezaji.
Machunda akiwa pamoja na wakuu wa idara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa amebainisha Uhusiano wa kimataifa uliopo baina ya Tanzania na China ulioanza tangu mwaka 1964 kuwa umezidi kupanuka kwa mashirikiano ya kiuchumi na wananchi wake wanadelea kunufaika nao.
"Kwa kutambua Mwanza ni kitovu cha biashara Serikali yetu imezidi kuimarisha njia kuu za uchumi ukiwemo usafiri wa majini, tuna Meli kubwa ya kisasa ya abiria iliyo mbioni kukamilika, Reli ya kisasa (SGR) iliyo pia kwenye hatua za mwisho kukamilika hivyo wawekezaji wanakaribishwa" Machunda.
Ameongeza pia miradi kama Uwanja wa ndege wa Kimataifa ambao Mandarasi anaingia site Mwezi huu kufanyia ujenzi pamoja na Madini ya kutosha huku akisisitiza kuwa wote wenye nia ya kuwekeza wanakaribishwa.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Huo Chengquan amebainisha ujio wao wa Mwanza ni kupata taarifa zitakazo washawishi kuja kufanya ushirikiano wa kiuchumi kutokana na wigo mpana wa sekta mbalimbali unaofanywa na kampuni yao.
"Nimefurahi kukutana nanyi na watu wanaoongoza sekta mbalimbali naamini tutashirikiana vizuri kuanzia kwenye afya, elimu na kwingineko," Amesema Mkurugenzi Chengquan.
Uongozi wa kampuni ya Henan Afro-Asia Geo-Engineering Ltd umeahidi kurudi Mwanza mwezi Septemba Mwaka huu kwa hatua zaidi za mashirikiano ya kiuchumi hususani kwenye sekta ya Viwanda, Kilimo, Afya, Elimu pamoja na biashara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.