Uhaba wa mashine za kisasa zenye uwezo wa kuchukua na kupima sampuli za damu katika hospitali nyingi nchini imekuwa moja ya changomoto kubwa katika sekta ya afya hapa nchini.
Mashine zilizokuwepo katika baadhi ya vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na zile za kanda zilikuwa ni zile mashine zenye uwezo mdogo na zilizokuwa zikichukua muda mrefu kutoa majibu ya sampuli zilizochukuliwa kupimwa. Ni ambazo kwa kiasi fulani zilikuwa zimepitwa na wakati (manual) na hivyo kuchelewesha upatikanaji wa majibu.
Ni wazi katika hali kama hii, hata usahihi wa majibu ya damu hayakuwa na uhakika kwa asilimia 100 na hivyo kuathiri utendaji kazi wa Mpango wa Taifa wa damu salama nchini.
Hata hivyo, kumekuwa na habari njema juu ya changamoto hii kwa sababu serikali sasa imeipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kununua mashine mpya za kisasa.
Habari hii imekuwa ni njema pia kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama ulio chini ya Idara ya Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambao unasimamia huduma ya damu salama nchini, zikiwemo kuhamsisha ukusanyaji damu kutoka kwa wachangia damu wa hiari na wa kujirudia, kupima magonjwa makuu manne, VVU, virusi vya homa ya ini B na C.
Mkoa wa Mwanza ni mmoja wa mikoa ambao itafaidika pia na mpango huu wa serikali.
Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa maadhimisho ya Siku ya wachangia damu duniani hivi karibuni, alisema kwa serikali imetoa a kibali kwa Bohari ya Dawa (MSD) Agosti 7 mwaka juzi cha kuanza mchakato wa kutafuta mashine za kisasa (Full Automation Machine) kwa mfumo wa kulipia vitendanishi ( Reagent rental system) ambazo zingewezesha kupima sampuli nyingi na kupata majibu yenye ubora kwa muda mfupi.
katika kukabiliana na changamoto ya ucheleweshaji wa majibu, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama sanjari na kuhakikisha upatikanaji wa damu salama ya kutosha kwa ajili ya kuokoa maisha ya wahitaji hapa nchini,
USIMIKAJI WA MASHINE
Katika utekelezaji wa hoja hiyo, Waziri Ummy anasema hadi sasa serikali imepokea jumla ya mashine 24, 12 zikiwa za kupima maambukizi katika damu na 12 za kupima makundi ya damu.
Anasema mashine hizo zimegawiwa kwenye vituo sita vya kanda hapa nchini, ambavyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Mtwara na Mbeya.
“ Kila kituo cha Kanda kimepatiwa mashine 4, mbili zikiwa ni za kupima magonjwa yanayoambukizwa kupitia damu ( Transifusion transmissible infections(TTI) na mbili ni za kupima makundi ya damu Blood grouping serology(BGS),” anaeleza.
Anasema kwa upande wa mashine za TTI vituo vya Mwanza na Dar es Salaam vimepatiwa mashine kubwa za kisasa aina ya Alnitis yenye uwezo wa kupima sampuli 150 ambayo ni sawa na vipimo 600 kwa saa moja.
“Vituo hivi vimepewa mashine hizi zenye uwezo mkubwa kutokana na ukweli kwamba ni vituo vinavyopokea sampuli kwa wingi kuliko vituo vingine vya kanda hapa nchini,” anasema.
Anasema mashine hizo mbili kubwa ambazo tayari zimesimikwa Mwanza na Dar es Salaam zimegharimu kiasi cha Dola za kimarekani 600,000 sawa na shilingi bilioni 1.4.
Anasema, aidha kila kituo kimpewa mashine moja aina ya Architect i2000 SR kama “backup” kutoka Kampuni ya Abbolt na vituo vingine vya Mtwara, Tabora, Kilimanjaro na Mbeya navyo vimepatiwa mashine mbili za aina ya Architect i2000 SR zilizogharimu kiasi cha dola za kimarekani 256,000 ambayo ni sawa na shilingi Milioni 600 na zina uwezo wa kupima sampuli 50 ambayo ni sawa na vipimo 200 kwa saa.
Kwa upande wa mashine za kupima makundi ya damu, Waziri Ummy anasema kila kituo kimepatiwa mashine mbili aina ya aina ya Neo Iris kutoka Kampuni ya Immucor zenye uwezo wa kupima sampuli 156 kwa masaa mawili.
Anasema kati ya mashine hizo, moja itakuwa ‘back up’. ambapo mashine hizo za kupima makundi ya damu zinagharama inayokadiriwa kuwa ni dola za kimarekani 150,000 kila moja ambayo ni sawa na shilingi 360,000,000., ambapo jumla ya gharama katika uwekezaji huo kwa mujibu wa Waziri Ummy ni sawa dola za Kimarekani 5,560,000 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 13.
“ Tayari mashine hizo zote za makundi mawili ya kupima damu na makundi ya damu zimeishafungwa katika kanda zote sita na mafunzo ya matumizi ya mashine hizi yhamefanyika kwa watumishi wa maabara kwa kanda tano,” anaeleza.
Anasema kuwa vile vile Mpango wa Taifa wa Damu salama umekamilisha uhakiki ubora wa mashine hizo katika baadhi ya kanda, hatua ambayo ni muhimu kabla ya kuruhusu matumizi ya mashine hizo.
Anasema zoezi la uhakiki wa ubora limekamilika kwa mashine za TTI’s katika kanda nne za mpango ambazo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, ambapo zoezi hilo la uhakiki limefanyika pia kwa kanda za Tabora na Mtwara.
Anaongeza kuwa Mpango wa Taifa wa Damu pia tayari umeishawasilisha maombi ya manunuzi ya vitendanishi MSD ya kiasi cha shilingi bilioni 9 kupitia fedha za Global Fund vya matumizi ya mwaka mzima na vitawasilishwa nchini kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.
“ Vituo vyote vya kanda vinapokea sampuli 25,000 kwa mwezi kwa sasa na Mpango wa Taifa wa Damu salama umeweka utaratibu wa kurudisha majibu kwa vituo vya afya na hosipitali ndani ya siku tatu tangu kupokelewa kwa sampuli,” anaeleza na kuongeza kuwa vituo vyote vya kanda kutokana na usimikwaji wa mashine hizo za kisasa vina uwezo wa kupima sampuli 60 kwa mwezi.
Anasema kuwa kutokana na MSD kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji na usafirishaji wa vitendanishi hakutakuwa na malalamiko tena juu ya ucheleweshaji wa majibu kwa kuwa mashine hizo zilizosimikwa zina uwezo mkubwa.
FEDHA ZAIDI KUTOLEWA
Katika kuimarisha ujenzi wa vituo vidogo vya uchangiaji damu, Waziri Ummy anasema tayari serikali imetenga shilingi bilioni 5 katika mwaka huu wa fedha katika ujenzi wa vituo hivyo.
Anasema kadri huduma za matibabu ya kibingwa zinavyoendelea kuboreshwa hapa nchini, ikiwemo ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, upandikizaji figo na upasuaji mwengine Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mloganzila, zimepanua wigo wa mahitaji ya upatikanaji wa damu salama.
“Jitihada zinafanyika ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa damu salama nchini, na lengo la serikali ni kumfikia kila mtanzania mwenye mahitaji ya damu salama popote alipo tuhakikishe anapata damu salama bila kikwazo chochote,” anasema, na kuongeza,
“Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria katika kila idadi ya watu 1000 zipatikane chupa 10 za damu, Watanzania tunakadiriwa tupo milioni 55 tunapaswa kupata asilimia moja ya idadi hiyo, hivyo chupa 550,000 zinahitajika kila mwaka kutosheleza mahitajina kwa ujio wa mashine hizi za kisasa hilo linawezekana ,” anaeleza
TAKWIMU ZA DAMU
Akifafanua kuhusu ulinganisho wa ukusanyaji wa damu hapa nchini, anasema mwaka 2016 zilikusanywa chupa 196,000, mwaka 2017 chupa 233,000 na 2018 idadi imeongezeka hadi kufikia chupa 307,000.
“Kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji damu, katika chupa 10 zinazohitajika kupatikana angalau tunapata chupa sita, hivyo nawasihi watanzania wote kujenga utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara ili tuweze kupata inayotosheleza,” anasema.
Anawataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanatekeleza agizo alilowapa la kuandaa kambi za wazi kwa ajili ya uchangiaji damu angalau mara tatu kila mwaka na watenge fedha katika bajeti zao kuwezesha ukusanyaji damu salama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.