Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amepongeza walimu, wanafunzi, wazazi pamoja na wadau wote wa elimu kwa jitihada zao zilizochangia kupanda kwa kiwango cha ufaulu mkoani humo.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa ushirikiano huo umeleta matokeo chanya katika sekta ya elimu ufaulu kwenye mitihani ya Kitaifa inayosimamiwa na NECTA kwa mwaka 2024 na 2025.
Ametoa pongezi hizo mapema leo tarehe 06 Agosti, 2025 katika hafla fupi ya utoaji tuzo na zawadi kwa waliofanikisha matokezo bora kitaaluma katika mitihani ya elimu msingi na sekondari pamoja na michezo kwa kipindi cha 2024 na 2025 mkoani humo ambapo Wilaya ya Ilemela imeibuka mshindi wa jumla.
Mhe. Mtanda amebainisha kuwa mwaka 2024 Mwanza imefanya vizuri katika mitihani ya NECTA ukilinganisha na 2023 ambapo kwa Darasa la Nne ufaulu ulikuwa 83% hadi 91%, Kidato cha Pili 87% hadi 89% Darasa la Saba 84% hadi 85%, Kidato cha nne 94% hadi 98% na Kidato cha Sita 2024 99.6% hadi 99.83 2025.
Aidha, ameeleza kuwa matokeo ya mitihani ya 2024 sio tu kwamba yameufanya Mkoa huo kufaulisha bali kutambulika kitaifa kwa kushika nafasi ya Sita kwa Elimu Msingi na nafasi ya Tatu kwa sekondari na kwamba kwa upande wa michezo Mkoa umeshika nafasi ya Kwanza kwa mara nne mfululizo.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa walezi na wazazi kushirikiana na walimu kusimamia kuwabakisha wanafunzi shuleni ili waondokane na utoro na tabia hatarishi zinazopeleka kupata mimba kwa kusimamia misingi ya sheria ya Mkakati wa malezi ya watoto.
"Wakati mwingine jamii inawaachia walimu au Wakuu wa Wilaya kusimamia miradi na fedha za maendeleo zinazoletwa kwenye shule kwa ajili ya kujenga miundombinu, tuache tabia hiyo na wazazi tushirikiane kusimamia ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo na maabara." Mkuu wa Mkoa.
Kadhalika, ametoa wito kwa jamii nzima kuhakikisha wanashiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa amani na utulivu na ametoa wito kwa viongozi kuhamasisha jamii kwa njia mbalimbali mathalani mabonanza katika kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kushiriki katika kuchagua viongozi.
"Vikombe hivi kwetu ni muhimu kwasababu vimeloa jasho la wanafunzi, walimu, Maafisa Elimu na Viongozi wa Wilaya, Halmashauri na Mkoa kwa pamoja wakiwa wanahakikisha taaluma Mwanza inakua juu." Amesema Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Mwl. Martin Nkwabi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.