UTOAJI WA CHAKULA CHENYE VIRUTUBISHO SHULENI NI LAZIMA: RAS BALANDYA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewataka wadau wa masuala ya Lishe Mkoani humo kuhakikisha chakula kinachopatikana kwenye shule za msingi na sekondari kinakua na virutubisho ili kutokomeza udumavu kwa watoto.
Ametoa wito huo mapema leo jumatatu ya Agosti 12, 2024 wakati akifungua Kikao kazi cha kujadili Afua za Lishe ambapo alibainisha kuwa suala la upatikanaji wa chakula kwenye shule za mkoani humo upo kwa asilimia 73 lakini ni asilimia 50 tu ndio kina virutubisho.
Bw. Balandya amefafanua kuwa kukosekana kwa chakula chenye virutubisho mathalani madini chuma na zinki pamoja na vitamini B 9 kumepelekea mkoa huo kuwa na udumavu kwa asilimia 27 kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwa utafiti wa mwaka 2022.
Amesema, wasindikaji wanaochakata vyakula ili kupeleka kwenye shule za Mkoa huo ni lazima wahakikishe vinakua na virutubisho na kwenye hilo amewaomba Shirika la Viwango (TBS) kupitia ofisi ya Kanda ya ziwa kuhakikisha wanasaidia kudhibiti ubora wa virutubisho kwenye vyakula hivyo.
"Ubongo na akili ya mtoto hutegemea lishe bora anayopatiwa hivyo twendeni tukawape chakula chenye virutubisho shuleni na tutoe elimu kwa wazazi na walezi kupitia vikao vya shule kuhakikisha wanawapa chakula bora nyumbani ili uwezo waliojaliwa na Mungu uonekane" Amesisitiza Balandya.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Jesca Lebba amesema ni vyema jamii ikajikita kwenye utoaji wa chakula chenye virutubisho ili kuwajengea watoto afya njema na kwa kufanya hivyo wtakingwa na tiba zitokanazo na udumavu au ukondefu ambavyo visipodhibitiwa jamii huingua kwenye kutibu maradhi.
"Afya bora ndio mtaji wetu wote, hatuwezi kufanya chochote bila kuwa na afya bora hivyo watoto wetu ni lazima wawe na lishe bora wakati wote ili tujenge Taifa lenye nguvu la sasa na la baadae." Ameongeza Mganga Mkuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.