*Vijana 194 wahitimu Mafunzo ya Atamizi Mwanza,watakiwa kutanua wigo wa kujiajiri
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewapongeza na kuwataka vijana walio hitimu mafunzo ya Atamizi kuziendeleza juhudi za serikali za kuongeza fursa ya ajira kwa vijana kwa kujiajiri na kuwaajiri wengine.
Mhe. Ulega ameyasema hayo leo Mei 29 wakati alipohudhuria hafla ya ufungaji mafunzo hayo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji yaliyo chukua muda wa Miezi 3 ambayo imewakusanyisha wahitimu 194 wa awamu ya kwanza kutoka katika vituo 14 nchi nzima iliyofanyika Mkoani Mwanza katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Butimba.
"Nipende kuwapongeza vijana mnaohitimu leo kwa hatua mliochukua ya kujifunza uvuvi kwa nia ya kuanzisha miradi ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji inachangia kwa kiasi kikubwa kukuza juhudi za serikali za kukuza fursa za ajira kwa vijana kupitia sekta ya uvuvi,"Amesema Mhe. Ulega.
"Kwa mwaka 2023/2024 wizara imepanga kuwawezesha vijana 750 kupata mafunzo kwa vitendo kwa vijana waliohitimu katika fani ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji nchini miongoni mwao watakua ni vijana waliopo katika mafunzo ya JKT." Mhe. Ulega.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Amos Makalla amesema sekta ya uvuvi inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza uchumi wa Mkoa wa Mwanza.
"Sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi kwenye Mkoa wa Mwanza shughuli ya uvuvi ni sehemu ya ajira kwa wananchi walio wengi kupitia biashara za samaki, kutengeneza vyombo vya kuvulia samaki na kwenye viwanda vya kuchakata Minofu ya samaki hadi kufikia Machi 2023 ambayo ni robo tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023 zaidi ya Shilingi Bilioni moja zilikusanywa kutoka sekta ya uvuvi zikiwa ni sawa na 31.125% ya makusanyo ya Mkoa",amesema Elikana.
Aidha, Bi. Happiness Meena, Naibu Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea Vijana ujuzi kwa vitendo zaidi ili waweze kuongeza ubunifu katika kile ambacho wamejifunza.
Vilevile, mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na wenye ulemavu Bi. Josephine Mwaijande amesema Ofisi yao ipo katika taratibu za kujenga kituo kimoja cha kutoa mafunzo hayo katika mwali wa Katongo Mkoani Kigoma
Pia, Bi. Jovina Eliam ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo kutoka Dar es salaam wakati akisoma Risala ameiomba serikali kuwapatia vitambulisho ambavyo vitawatambulisha kama wataalam na wabobezi wa maswala ya uvuvi na kuwatofautisha na wale ambao watakua hawajabobea katika mafunzo hayo
Lengo la mafunzo hayo ya ATAMIZI ambayo yamechukua ni kuwajenga vijana walio hitimu fani ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji ni kuondoa dhana ya kuajiriwa na hivyo kuweza kubuni miradi na kuanzisha kampuni hivyo kuchangia katika pato la Taifa na kutoa fursa za ajira kwa watanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.