VIJANA MWANZA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI
Serikali Mkoani Mwanza imewataka Vijana wa Mkoa huo kuchangamkia fursa mbalimbali ili waweze kupata kipato kitakachowasaidia kujikwamua na umaskini pamoja na kuboresha hali ya maisha.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Machi 29, 2025 alipokuwa akizungumza na Vijana walioshiriki katika Kongamano la PPRA linalohusu Fursa za Kiuchumi Mkoani Mwanza.
Mkuu wa Mkoa amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira mazuri ya kuimarisha vipato vya wananchi wote kupitia Mifuko ya Maendeleo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ambapo kwa sasa dirisha la mikopo limefungwa tangu Oktoba, 2024.
Aidha Mhe. Mtanda amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, imezitaka Taasisi zote za Serikali kutenga Asilimia Thelathini ya bajeti zake kwa ajili ya Makundi Maalum (Wanawake, Vijana, Wazee na Watu Wenye Ulemavu).
“Kiasi hiki ni kwa ajili ya Watanzania ambao wanaweza kujikusanya na kuunda vikundi rasmi vya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, kisha washiriki kwenye tenda za Serikali”.
Ninawasihi sana, mfuatilie kwa makini taarifa mtakazopewa katika Kongamano hili, ili mfahamu jinsi ya kupata sehemu ya fedha hizi kupitia Mfumo wa NeST, na kujiinua kiuchumi. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Naye Mkurugenzi wa Generation Samia, ambaye pia ndiye mratibu wa kongamano hilo Bw. Omary Kimweri amesema wao kama Kizazi cha mfanikio au maarufu kama Generation Samia wamedhamiria kuyaunganisha makundi mbalimbali na fursa zinazotengenezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Ndugu Dennis Simba, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) amesema fedha hizo 30% Serikali ya Dkt. Samia sio fedha chache ni nyingi sana ambapo ni zaidi ya trilioni 5 kwa bajeti ya mwaka mzima
Kadhalika ameahidi kuendelea kutoa elimu ili makundi hayo yaweze kujipanga kwa kutafuta fursa mbalimbali na amesema mpaka leo ni takribani trilioni 15 zimekwisha tolewa tangu kuanza kwa sheria hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.