Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amewataka watendaji wa elimu mkoani humo kuweka mikakati ya kupandisha ufaulu hasa kwenye somo la Hisabati na kuondoa kabisa wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwenye shule za Msingi.
Ndugu Elikana ametoa rai hiyo wakati
akifungua Kikao kazi cha watendaji wa Elimu kuanzia ngazi za Kata hadi Mkoa waliokutana kwa ajili ya kufanya Tathmini ya matokeo ya Kuhitimu Elimu ya Msingi na Sekondari 2022 na mitihani ya upimaji ya darasa la nne na kidato cha pili kutokana na ufaulu kushuka kwa elimu msingi kwa asilimia 0.6.
"Hisabati ni somo la msingi sana kwa kuendelea mbele kimaisha hivyo lazima tuweke mikakati ya kufaulisha somo hili katika madarasa yote, na uzuri wa somo hili ni kwamba mtoto akipata alama Mia Moja basi mwalimu atampatia mtoto huyo mia moja kwahiyo ndilo somo rahisi ukilizingatia." Amesema Elikana.
Amefafanua kuwa watoto zaidi ya asilimia 70 wamefeli somo la hisabati hivyo ni lazima walimu wa somo hilo wawe na mikakati ya kufaulisha kuanzia darasa la kwanza na kwa walimu wa kuanzia darasa la tatu kuweka mkakati wa watoto kufanya vizuri kwenye somo la kiingereza ambalo nalo limekua kikwazo.
Vilevile, ametoa wito kwa wataalamu hao kutumia kikao kazi hicho kuweka mpango wa kuwa na chakula cha mchana kwa wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari kwa kutumia wazazi na wadau kwani watoto wanaposhinda na njaa ndipo wanakosa uwezo wa kufanya vizuri kwenye masomo yao.
"Serikali inaweka nguvu kubwa sana katika kuhakikisha kila mtoto anayestahili kwenda shule basi aende shule ndio maana kwenye kila wilaya imejenga madarasa ya kutosha hivyo ni lazima sisi viongozi wa elimu tuhakikishe watoto wote wanaostahili kwenda shule kuanzia shule za awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanakwenda shule." Amesema Katibu Tawala.
Awali Akimkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa, Afisa Elimu Mkoa Martine Nkwabi alibainisha kuwa Kikao kazi hicho ni maalumu kwa ajili ya kufanya Tathmini ya matokeo ya mitihani ya taifa na upimaji 2022 ambapo kwa mwanafunzi ufaulu umeshuka na akafafanua kuwa utafanyika upimaji katika ngazi zote kuanzia kwenye kata ili kukuza ufaulu kwa watoto.
"Ndugu viongozi wenzangu, matokeo ya Mitihani ya Kuhitimu Elimu ya Msingi na Sekondari na hata ya Upimaji tumeshuka kitaifa na kimkoa hivyo kuna haja kwa sasa tunapoanza mwaka mpya wa 2023 kuweka mikakati ya kuona namna gani tunatoka hapo na kutekeleza maelekezo ya TAMISEMl juu ya usimamizi bora wa Elimu." Afisa Elimu amesisitiza.
Afisa Elimu amesema anasikitishwa na uwepo wa wanafunzi 23,900 wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu wakiwa kwenye madarasa ya kuanzia darasa la pili hadi la saba pamoja na agizo lake la kuhakikisha inawekwa mikakati thabiti ya ufundishaji ndani ya siku 90 kuanzia mwezi Agosti 2022 alipotoa agizo hilo.
"Wito wangu kwa wazazi ni kuhakikisha wanafunzi wa Awali, darasa la kwanza na wale 85300 wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023 waingie shuleni kati ya januari 09 hadi 15, 2023 ili wapate utangulizi wa masomo ya kiingereza na umahiri wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu." Amesisitiza Afisa Elimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.