Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella amewaasa viongozi kuhakikisha kuwa katika kila jambo wanalolifanya waache alama ili wale wanaowaongoza waige mfano bora katika utendaji wao wa kila siku ikiwa ni pamoja na kuwa wabunifu na kufanya vitu tofauti ili kuleta maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mhe.Mongella ameyasema hayo wakati akifungua semina ya viongozi ngazi ya Mkoa hadi Halmashauri inayofanyika katika Ukumbi wa NIMR (MITU) kuanzia julai 2 hadi 4 ikijumuisha Waheshimiwa wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi,makatibu tawala wa Wilaya,waweka Hazina wa Halmashauri na baadhi ya Makatibu tawala wasaidizi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kuratibiwa na UONGOZI Institute kutoka Makao Mkuu Dar es Salaam.
"Kiongozi ni mfano, mtatuzi wa changamoto na mtoa mwelekeo wa taasisi husika lazima aache alama,afanye vitu tofauti kwa maendeleo ya taasisi, jamii na Taifa kwa ujumla,alisema Mhe.Mongella.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa TAKUKURU Dkt. Edward Hoseah akiwasilisha mada yake ya Uongozi wa Uadilifu amewaasa viongozi kuhakikisha wanasimamia,kulinda na kuangalia maslahi mapana ya Taifa na watu wengine na siyo maslahi yao wenyewe.
"Kiongozi muadilifu ni lazima awe mtu anayeamini katika haki na kufanya maamuzi magumu kwa kuzingatia taratibu sahihi na awe na ndoto na maono yanayotekelezeka,"alisema Dkt.Hoseah.
Dkt.Hoseah ameongeza kuwa hatuwezi kuwa na maendeleo kama hakuna viongozi waadilifu na kusisitiza kuwa ukiwa kiongozi muadilifu lazima kutakuwa na kitu kinachokupelekea kufanya jambo linavyotakiwa lifanyike kwani uadilifu huleta amani na mafanikio katika Taasisi,Jamii na Taifa zima.
Pamoja na kusisitiza maendeleo Dkt.Hoseah amezitaja mbinu za kupambana na rushwa na kusema kuwa lazima kuwe na utashi wa kisiasa na uadilifu, mfumo imara wa uadilifu wa kitaifa pamoja na usawa, kwa maana kuwa waliopo Serikalini hakuna anayependelewa. Vivyo hivyo kuhusisha mfumo mzima kwa ukamilifu yaani Serikali isifanye kazi peke yake.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu Taasisi ya UONGOZI Bw. Kadari Singo katika ukaribisho alitumia muda huo kuwakumbusha viongozi umuhimu wa kufahamu na kufuata itifaki mbalimbali.Aidha alitoa mfano wa utoaji business card,ambapo alisema kiongozi wa ngazi ya chini haruhusiwi kumpatia business card kiongozi wa juu,ila pale tu anapoombwa kufanya hivyo.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Said Kitinga akachangia kuhusu namna mifumo na Sheria zilizopo Sasa zinavyojikita zaidi kumlenga mtu aliyepokea rushwa na kumwacha yule aliyetoa rushwa. Na kwamba Kama Taifa tutafakari ni jinsi gani tutaibadilisha mitazamo ya jamii ya kitanzania ambayo inamuona kiongozi aliyemaliza muda wake bila kujipatia utajiri,Kama mtu aliyeshindwa kunitumia nafasi yake vizuri. Hivyo kuihalalisha rushwa ndani ya jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.