Selikali mkoani Mwanza imesema ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo (machinga) kwa mfumo wa kidijitali ni mkakati wa Rais John Magufuli, kuwapa nguvu wanyonge watoke kwenye umasikini na hali duni za maisha.
Pia kutokana na zoezi hilo kuwa nyeti imeagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kusimamia kwa weledi na umakini zoezi hilo ili kuwe na tija.
Agizo hilo liilitokea jana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, wakati akizungumza na Wakuu hao wa Wilaya,Wakurugenzi wa halmashauri na maofisa biashara kutoka wilaya saba za mkoa huo .
Alisema zoezi la kuwapa vitambulisho wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, ni mkakati wa Rais Magufuli wa kuwapa nguvu za kiuchumi wananchi wanyonge na kuwafanya watoke kwenye hali duni ya umasikini na kupata hali bora zaidi.
Mongela alisema mfumo huo wa vitambulisho unalenga kujenga uwezo wa wananachi wetu, utambuzi wa matatizo ya wafanyabiashara hao na jinsi ya kuwasaidia kukuza uchumi wao na uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Alisema zoezi hilo nyeti lilianzishwa na Rais Magufuli kwa makusudi kwa ajili ya kuwainua wanyonge kiuchumi hivyo ni vyema likakamilika mapema na kwa wakati ikizingatiwa Mwanza haijawahi kuchelewa.
"Mwanza tumepewa vitambulisho 84,000 hadi kufikia Julai,Mosi mwaka huu viwe vimewafikia walengwa wote, Mwanza hatujawahi kuchelewa kwenye zoezi hili hivyo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maofisa biashara nendeni mkasimamie kwa weledi na umakini jambo hilo nyeti liwe na tija, " alisema Mongela.
Alifafanua mgawo wa kila halmashauri za wilaya ambapo Wilaya ya Nyamagana na Jiji la Mwanza imepewa vitambulisho 23,000, Ilemela 20,500 , Ukerewe 5,500 huku Halmashauri za wilaya za Buchosa, Sengerema,Magu, Misungwi na Kwimba zikipewa kila moja vitambulisho 7,000.
Kwa mujibu wa Mongela, mfumo uliowekwa mwaka huu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ndiyo watakaowajibika kuvigawa vitambulisho hivyo vitakavyokuwa na pia pamoja taarifa zote muhimu za kila mfanyabiashara mdogo atakayesajiliwa kwenye mfumo kama ilivyo kwa leseni za udereva .
Aidha kabla ya vitambulisho hivyo kuanza kugawiwa maofisa biashara na wataalamu wa Tehama walizopata mafunzo wanalalamika kutoa elimu ya matumizi ya mfumo kwa watendaji wa mitaa, vijiji na kata ili waweze kuwahudumia kwa ufanisi wafanyabiashara hao wadogo ambapo mwaka jana Mkoa wa Mwanza ulipokea vitambulisho 88,000 vyenye thamani ya sh. bilioni 1.76.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.