Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella amekabidhi vitambulisha 15,000 kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nane za mkoa huo ili vitolewe kwa wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) wa mkoa huo.
Vitambulisho hivyo vilivyokabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ndg. Joseph Mtandika ni sehemu ya vitambulisho 88,000 ambavyo mkoa huo umepangiwa na Ofisi ya Rais kwa ajili ya kuwapatia wafanyabiashara ndogo ndogo.
Utaratibu wa utoaji vitambulisho hiyo ni mpango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli wa kuwatambua wamachinga wote ili kuwaondoa katika usumbufu mbalimbali waliokuwa wanaoupata.
Katika makabidhiano hayo kwa wakuu wa wilaya, Mhe. Mongella amesema kwamba zoezi la ugawaji vitambulisho hivyo kwa mwaka jana lilikuwa la mafanikio makubwa na kwamba anaamini mwaka huu litakwenda vizuri pia.
“Vitambulisho hivi vimeondoa adha ya usumbufu kwa wamachinga. Katika ugawaji wa mwaka jana tumejifunza mengi, tutumie sasa uzoefu wa mwaka jana kufanya vizuri zaidi,” amesema.
Awali Meneja wa TRA alisema kwamba idadi ya vitambulisho kwa mkoa wa Mwanza umeongozwa kwa asilimia tano, kutoka 80,000 vya mwaka jana hadi 88,000 na imetokana na mafanikio makubwa katika usambazaji wake mwaka jana kwa wamachinga.
Akaongeza, “...Pia vitambulisho vya sasa vimeboreshwa zaidi kwa kuweka serial number (mpangilio maalum wa namba) na zipo katika mtandao hivyo inakuwa rahisi kwa sasa kujua kitambulisho hiki ni cha mkoa gani.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.