Serikali imesema vyombo vya habari ni nguzo kubwa ambayo husaidia kutimiza mipango ya maendeleo ya kila mwaka huku ikiwataka waandishi wa habari kuitangaza nchi na vivutio vyake kwa lengo la kuongeza watalii wa ndani na nje.
Kauli hiyo imetolewa jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini, Dkt. Maurus Msuha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Aldof Mkenda wakati akifunga mkutano wa mwaka wa wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali nchini ulioandaliwa na Shirika la Higadhi za Taifa (TANAPA).
Dkt. Msuha alisema vyombo vya habari ndio nguzo kuu inayotegemewa na Serikali kwa ujumla kuwafikishia ujumbe kwa umma kwa haraka juu ya jambo lolote linaloendelea, hivyo waandishi wa habari wanapaswa kutambua nafasi yao katika kulitetea na kulitangaza taifa lao kwa kutanguliza uzalendo.
“Hadi leo tunafunga mkutano huu umekuwa wa kipekee kutokana na kuwa na idadi kubwa ya washiriki tofauti na mikutano iliyotangulia tuliyofanya, kwanza umeongeza tija ya ufahamu wa hifadhi zetu sasa kilichobaki twende tukavitangaze vivutio vyetu na kuhawamasisha jamii kufanya utalii wa ndani.
“Pia kwa kutumia vyombo vyenu, andikeni habari zinazosaidia kuongeza watalii kutoka nje ukizingatia sekta ya utalii ndio inaongeza kuingiza fedha za kigeni nchini kwa asilimia tano, pia inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.6 huku ukitoa ajira za kudumu zaidi ya 500,000 na zisizo rasmi ni milioni mbili.
“Tambueni Serikali inategemea sana vyombo vya habari na ni nguzo kubwa inayotufanya kutimiza mipango ya maendeleo inayoibuliwa, imani yetu wote mliohudhuhuria mkutano huu mtakuwa mabalozi wetu katika wizara hii ya maliasili na utalii, “alisema
Dkt. Msuha alisema inawezekana kabisa waandishi wakapata taaifa ambayo kwa mujibu wa taaluma yao ni habari ya nzuri inayoweza kuwaingizia kipato lakini akaomba wahariri kufikia maslahi mapana ya taifa endapo taarifa hiyo itatangazwa, hivyo aliomba kutanguliza uzalendo kwanza kama ilivyo kwa mataifa makubwa yaliyoendelea kutotangaza habari inayobomoa nchi yao.
Wakitoa michango na mapendekezo yao, baadhi ya wahariri na waandishi wa habari walisema mfumo ilioanzishwa na Tanapa kukutana nao kila mwaka umesaidia kuelewa mambo mbalimbali ya wizara ya maliasili na utalii na kuondoa ukiritimba uliokuwapo hapo awali.
Bakari Kimwaga alisema Tanapa ni miongoni mwa taasisi ya Serikali ambayo imeonyesha njia sahihi ya kushirikiana na vyombo vya habari nchini na kuzishauri wizara zingine kuiga mfano huo kwani utasaidia kuijenga Tanzania kiuchumi na kuleta sura ya umoja.
Kimwaga aliishauri Tanapa na taasisi zingine kutumia fursa ya ndege Tanzania kuweka vijarida vya matangazo ya vivutio vyetu ili zinapofanya safari za nje na ndani ya taifa, abiria waweze kusoma na kutambua kilichopo na kufanya utalii.
Alisema miaka 50 ijayo mahitaji ya binadamu yatakuwa makubwa kuanzia maji, umeme, chakula , hewa na vitu vingine na endapo Tanzania itachukua hatua mapema ya kulinda rasilimali zilizopo itakuwa taifa tajiri kwa sababu ya uwepo maji ya baridi ambayo pengine watanzania wanaweza kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji mara tatu kwa mwaka na kuachana na kutegemea mvua.
Alisema sekta ya utalii ndio inaongoza kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia tano, hivyo ni dhahiri inapaswa kutunza kikamilifu.
Naye Kamishna wa Tanapa, Allan Kijazi alisema hifadhi za taifa zilizopo kaskazini ndiyo zinaongoza kutembelewa na watalii tofauti na kanda zingine ambapo kama Serikali imepanga kufanya mageuzi ili hifadhi zingine ziweze kufahamika zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.