Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Christopher Kadio amewataka wadau wa kilimo kutoa mawazo, michango na mapendekezo bora na makini yatakayo saidia kurekebisha sera ya kilimo ya Taifa ya Mwaka 2013.
Kadio alitoa wito huo alipokuwa akifungua kikao kazi cha wadau wa kilimo kuhusu kujadili na kutoa maoni ya marekebisho ya sera hiyo.
Alisema, Sera ya kilimo inatoa mwongozo wa jumla kuhusu mwelekeo wa masuala ya kuzingatia katika jitihada za uendeshaji wa sekta hiyo.
“Sera hii ilikuwa katika utekelezaji karibu miaka sita sasa na masuala mengi mapya yamejitokeza katika ngazi mbalimbali kuanzia ya kimuundo ,kisekta,kitaifa na kimataifa hivyo hali hiyo inahitaji kuiangalia upya sera ya kilimo iliyopo ili kuendana na hali halisi ilivyo sasa”alisema Kadio.
Kadio ameongeza kuwa, Sekta ya kilimo inatoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5 ikichangia karibia asilimia 30 ya pato la Taifa kwa mwaka 2018 ambapo sekta ndogo ya mazao ilichangia asilimia 16.58.
“Sekta ya kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda na kuchangia karibu asilimia 100 ya mahitaji ya ndani ya chakula, hivyo ni vyema ikawa na muongozo thabiti”alisema Kadio.
Profesa Msataafu wa Uchumi na Kilimo Lucian Msambichaka alisema ili kilimo kiwe na tija ni lazima miundombinu ya umeme, uchukuzi na maji iboreshwe.
Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo Obey Assery alisema, maeneo waliotilia mkazo kwenye sera hiyo ni mrorongo mzima wa tija, kuanzia matumizi bora ya ardhi na pembejeo kwa maana ya mbolea, mbegu bora na viuatilifu.
Aidha, Ofisa Kilimo Wilaya ya Ilemela Neema Semwaiko alisema, ili sera iwasaidie wakulima kipengele cha ugani kiimarishwe kwakuwa wagani ni wachache na vifaa wanavotumia vimepitwa na wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.