Wadau hao wamekutana leo katika kikao kilichofanyika jijini Mwanza na kuhudhuriwa na taasisi za kifedha, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya serikali, Makampuni ya huduma za pembejeo na zana za kilimo pamoja na Makampuni ya usindikaji, na kuongozwa na mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. John V. K Mongella huku dhumuni likiwa ni kuwakutanisha wadau hao ili kuweza kubadilishana ujuzi wa kazi wanazozifanya.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Mongella amewaeleza wadau hao kujikita katika kilimo cha mazao ikiwemo kilimo cha alizeti, pamoja na kilimo cha pamba na kujiuliza swali, nimefanya nini katika kukuza sekta za kilimo, uvuvi na mifugo.
" Nipende kuwashauri wadau kujikita hasa katika kilimo cha mazao, ikiwemo kilimo cha alizeti mamoja na kilimo cha pamba".
Aidha Mhe. Mongella amebainisha kuwa sekta ya kilimo imekuwa na mipango ya kuondoa umaskini, kuongeza usalama wa chakula na kuongeza pato.
"Sekta ya kilimo ina mpango wa kuondoa umasikini, kuongeza usalama wa chakula, ubora wa lishe na kuongeza pato kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, kwenye kaya, jamii mpaka taifa,"alisema Mongella.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio amebainisha kuwa kikao hicho kitatoa nafasi kwa wadau mbalimbali kupata fursa ya kufahamu changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo katika mkoa wa Mwanza.
"Wadau mbalimbali watapata fursa ya kufahamu changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika mkoa wetu wa Mwanza,"alisema Kadio.
Aidha Meneja wa Benki ya NMB tawi la Pamba Road, Dotto Alex Makota, ameeleza kuwa wanashiriki kikamilifu katika huduma za kifedha kwenye kilimo kwa kutoa mkopo wa pesa katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha wakulima wananufaika.
"Sisi kama NMB tunashiriki kikamilifu katika huduma za kifedha kwenye kilimo, na asilimia 35 ya pesa ya NMB inakwenda katika kilimo kwa kutoa mikopo kwa wakulima," alisema Makota.
Aidha Mwenyekiti wa wafugaji Wilaya ya Sengerema Clement Mathayo amebainisha changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo ikiwemo kukosekana kwa maeneo ya kutosha kwa ajili ya malisho, maji na kukosekana kwa soko la uhakika.
"Wadau wa ufugaji tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosa soko la uhakika, maeneo kwa ajili ya malisho na maji, tunaomba Serikali itutazame kwa upana,"lisema Mathayo.
Pamoja na hayo Mhe. Mongella amewashauri viongozi kuweza kutoa nafasi kwa wananchi wao ili kuweza kuzungumza na kueleza changamoto zinazowakabili katika sekta mbali mbali wakati wa vikao vyao na wananchi, pia amewataka wadau kuwa mfano kwa kuweza kutekeleza majukumu yao kwa vitendo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.