Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameutaka uongozi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokuwa wanafanya biashara Stendi Kuu ya zamani ya mabasi yaendayo mikoani ilipojengwa mpya katika Kata ya Nyegezi wapewe kipaumbele kupata maeneo ya kufanyia biashara.
Mhe.Majaliwa ametoa agizo hilo Oktoba 17,2022 wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa stendi hiyo inayojengwa kwa fedha za serikali Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kwa gharama ya Sh bilioni 15,885,589,063 na mkandarasi Mohammedi Builders Ltd.
"Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati lengo ni kuwanufaisha wananchi wake na mmeniambia kwamba mmejenga stendi hii nzuri kabisa ya kifahari lakini kuna eneo limebaki hivyo endapo maeneo yaliyopo ndani ya stendi hii yatakuwa machache kuwatosha wafanyabiashara wote waliokuwa wakifanya biashara zao hapa awali wajengeeni kwenye eneo hilo.
" Maana Rais Samia Suluhu Hassan ameleta Shilingi bilioni tisa katika jiji la Mwanza kwa ajili ya kujenga masoko nia na dhimira yake ni kuwaandalia na kuwajengea machinga maeneo yao ili wafanye biashara zao katika mazingira bora, amesema na nyie wafanyabiashara mliokuwa mnafanya biashara kwenye stendi hii zamani kabla ya ujenzi wa hii mpya haujaanza kama kwa sasa hautafanya tena biashara toa taarifa kwenye uongozi wa jiji ili wengine wanaohitaji wagawiwe maeneo usikae kimya,"ameagiza Mhe. Majaliwa.
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza wajipange kwa ajili ya
kunufaika na miradi mikubwa ya kimkakati inayojengwa mkoani humo ikiwemo ujenzi wa Reli ya kisasa(SGR), daraja la kigongo busisi maarufu kama Daraja la J.P Magufuli, stendi hiyo ya Nyegezi na iliyojengwa Wilaya ya Ilemela ambapo amewahakikishia wananchi kwamba hakuna mradi wowote wa kimkakati unaotekelezwa ndani ya mkoa huo utakaokwama maana fedha zipo na tayari serikali imeishazitenga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Yahya Sekiete amesema hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 98 ingawa ulikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo kutokana na kupanda kwa bei, bati za geji 26 zilizokuwa hazipatikani nchini pamoja na baadhi ya vifaa vinavyoagizwa nje ya nchi kuchelewa kufika bandarini.
" Mradi huu ulianza kutekelezwa Februari 5, 2019 ukikamilika utasaidia kuongeza mapato ya halmashauri ya jiji la Mwanza hivyo kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu pia utalifanya jiji la Mwanza kuwa la kisasa zaidi, utasaidia kukua kwa biashara nyingine kutoka mikoa mbaimbali na nchi jirani.
Ametaja maeneo yatakayokuwepo baada ya mradi huo kukamilika kuwa ni pamoja na eneo la maegesho ya mabasi 120, madogo 80 kwa wakati mmoja, maduka makubwa 14, madogo 60, sehemu tatu za abiria wapatao 7400 kusubiria mabasi, vyoo saba vyenye matundu 63 jengo la abiria, benki, vibanda 38 vya kukatia tiketi na vibanda vya mama lishe na eneo maalum kwa ajili ya wanawake wanaonyonesha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.