“Nimekutana na bomu na maajabu hapa Mwanza” ndiyo kauli ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aliyoitoa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na Wakuu wa idara zote zilizo chini yake katika kikao cha majumuisho ya ziara yake mkoani Mwanza.
Waziri Kamwelwe alisema licha ya mambo makubwa ya maendeleo kufanyika lakini bado baadhi ya maeneo yanatia shaka, uzembe na kuwa na dalili za uhujumu uchumi hususan katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na reli, kwanini wahujumu hawa wasifichuliwe hatua zikachukuliwa dhidi yao.
Mhe. Kamwelwe ameongeza kuwa, dreamline ni ndege kubwa inatua viwanja vine tu hapa Tanzania kikiwamo cha Mwanza ingawa kuna mambo ya kurekebisha haraka kabla ya kutua hapa Julai 29, mwaka huu lakini nisema wazi nimekutana na maajabu katika ukataji wa tiketi, yaani ATCL haina dirisha maalum la kukata tiketi zake badala yake wanatumia mawakala.
“Mawakala wale hawana ofisi bali wana vibanda tu, haitoshi bei ya tiketi ya chini kabisa inakatwa zaidi ya 400,000 wakati sisi tulielekeza iwe Sh 190,000, vile vile mawakla wale inaelezwa wana mikataba ya ajira na kampuni nyingine, kwa hiyo hapo kuna hali ya kuhujumu ndege zetu na shirika likafa tena,”alisema Kamwelwe.
Alisema moja ya maeneo ambayo hakuridhika nayo ni namna ya ukataji wa tiketi za abiria unavyofanyika kwa kuwatumia mawakala ambao hawana ofisi maalum ispokuwa wanatumia vibanda huku bei elekezi ya chini kabisa kwa ndege za shirika hilo ni Sh 190,000 lakini wao huongeza na kufikia kiasi cha Shilingi 400,000 na 450,000.
“Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ilikuta shirika hili halipo hai lakini leo hii limefufuliwa na kuwa na ndege zake ambapo juzi tumeshuhudia tukipokea ndege kubwa ya dreamline yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 260, pia tunazo ndege za bombardier tatu.
Waziri Kamwelwe aliwataka viongozi wanaohusika kumpa maelezo ya kina juu ya bei hizo kabla ya kuchukua hatua zaidi ambapo ameelekeza kufanyika haraka mfumo wa uboreshaji na uthibiti wa ukataji tiketi.
“Kuna hali ya hujuma na hatuwezi kubembelezana katika suala hilo na sipo tayari kuona jitihada za Rais Dk. John Magufuli zinakwamishwa na watu wachache, naomba mfumo huo uanzishwe ndani ya wiki mbili, naweza kuchukua hatua muda huu baadaye mkanilaumu mimi ndiye nimewaingilia ndiyo maana nimesema nahitaji maelezo kwanza,”alisema Kamwelwe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.