WAGONJWA KIPINDUPINDU MWANZA WAPUNGUA-RC MAKALLA
*Asema kuna mpya 1 na waliolazwa 7 tu Mkoani Mwanza*
*Awataka TARURA kuondoa maji yaliyotuama kwenye mitaro*
*Asema kwenye mikusanyiko tuzingatie usafi na kanuni za afya kutokomeza Kipindupindu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema Maambukizi ya ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani yamepungua sana kwani kuna mgonjwa mpya mmoja tu ambapo saba pekee wakiwa hospitali wamelazwa kwenye maeneo mbalimbali na akawataka wadau kuendelea na mikakati ya kuthibiti kusambaa.
Mhe. Makalla amebainisha hayo mapema leo Januari 24, 2024 wakati wa mkutano wake na Mganga Mkuu wa Serikali,Prof.Tumaini Nagu uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huku ukiwakutanisha viongozi wa Taasisi mbalimbali za Serikali za Mkoa huo.
Makalla amesema ni lazima kuendelea na mikakati ya kuthibiti kusambaa kwa maradhi hayo huku akitaja afua ya kuzibua mitaro ili maji ya mvua yasituame na kufikia hatua ya kusambaa kwenye makazi ya watu.
Akibainisha namna tatizo hilo lilivyo dhahiri Makalla amesema tangu kuibuka kwa ugonjwa huo juhudi mbalimbali zimefanywa kuudhibiti na akatumia wasaa huo kukemea tabia ya kuishi kwa mazoea hususani kwenye tabia za ulaji wa vyakula bila kuosha hasa Matunda.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewataka wadau wa afya na viongozi wengine kuzingatia sheria ndogondogo za Serikali za mitaa ili kuhakikisha afya ya jamii inazingatiwa hususani kwenye makundi kama ya mialo ya uvuvi.
"Ukiugua kipindupindu maana yake umekula mavi mabichi, aidha kwa uchafu kupitia kula kinyesi chenyewe au kupitia vitu mbalimbali tunavyoweka mdomoni kwa mikono isiyo safi, hivyo ni lazima watu wanawe mikono kwa maji safi na salama tena kwa Sabuni wakati wote" Prof. Nagu.
Halikadhalika, Mganga Mkuu ametoa wito kwa jamii kula vyakula vya moto, kuosha matunda na kunawa mikono kwa naji safi na salama yanayotiririka na kwa sabuni ili kukomesha kabisa janga hilo ndani ya Mkoa na ukanda huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.