Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka wakuu wapya wa wilaya za nyamagana na ilemela kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ili kuondoa aibu ya jiji la mwanza na manispaa ya ilemela kuwa miongoni mwa halmashauri nchini zilizofanya vibaya kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mhe.Mongella ametoa agizo hilo wakati wa hafla ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za Nyamagana,Ilemela,Magu na Ukerewe ambapo pia amewataka kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika halmashauri hizo.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya walioteuliwa ni Dkt, Severine Mathias Lalika (Ilemela), Mhe. Dkt Philis Mishack Nyimbi (Nyamagana), Mhe.Dkt.Philemon Sengati Lugumiliza (Magu) na Mhe. Cornel Lucas Boniphace Magembe (Ukerewe).
Aidha,Mhe.Mongella aliwakabidhi vitendea kazi ambavyo ni Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, Sheria za serikali za mitaa (a) Mamlaka ya wilaya (Sura ya 287) na marekebisho yake(b)Mamlaka ya miji(Sura ya 288) na marekebisho yake, Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 na marekebisho yake, Mwongozo wa uwekezaji wa Mkoa wa Mwanza wa mwaka 2017,na Masharti ya kazi ya Mkuu wa wilaya ya mwaka 2016.
“Fanyeni kazi kwa juhudi na ushirikiano kwa kusimamia utendaji kwenye Wilaya pia zingatieni ukusanyaji wa mapato na muwe wabunifu na kuacha mizaha kwa kupiga vita uvuvi haramu,komboeni majimbo na kuboresha mazao ya pamba,mpunga na harizeti,”alisema Mongella.
Awali aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Hadija R.R. Nyembo akitoa hotuba kwa wakuu wa Wilaya wanaoanza na kuwaasa kuwa wasisite kuuliza pale penye utata pia wafanye kazi kama timu moja ili kuleta ufanisi na matokeo mazuri kwa wananchi.
Kwa upande wao wakuu wa Wilaya walioapishwa wamesema kuwa wanahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi waliostaafu pamoja na wananchi na kuahidi kusimamia maendeleo ya uchumi na viwanda ili kuwainua wananchi kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.