Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela leo tarehe 03 februari, 2023 amewaapisha Wakuu wa Wilaya za Ukerewe na Magu kufuatia Uteuzi wa Wakuu wa Wilaya uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania januari 25, 2023.
Akizungumza kwenye hafla ya kuwaapisha Wakuu hao wa Wilaya Mhe. Hassan Bomboko (Ukerewe) pamoja na Mhe Rachel Kasanda (Magu) Mhe. Shigela amewataka kushirikiana na viongozi wengine kusimamia vema masuala ya Utawala bora kwenye maeneo yao kwa kuzingatia namna ya uendeshaji wa taratibu za nchi kwa mujibu wa sheria.
Aidha, amewataka wakuu hao wapya wa wilaya na wale wanaoendelea na majukumu kwenda kusimamia maadili yao binafsi na ya watumishi wa umma katika kuhakikisha mienendo yao katika kuhudumia wananchi inaenda sambamba na utawala bora unaozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.
Vilevile, amewataka kwenda kusimamia kwa dhati masuala ya Usalama wa Wananchi kwenye wilaya zao kwa kuhakikisha wananchi wanaishi kwenye Mazingira Safi na Salama kwa Afya za kila siku na kwa kutatua migogoro inayotokana na sekta za Biashara, Uvuvi, Kilimo, Elimu na Miundombinu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Sixbert Reuben amewapongeza Wakuu wapya wa Wilaya kwa kuaminiwa na kupata Uteuzi na amewaahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwenye Chama hicho katika kutimiza majukumu ambayo Mhe. Rais amewaamini na kuwapa jukumu la kutekeleza ndani ya Mkoa wa Mwanza.
"Mmepewa jukumu kubwa sana hivyo nendeni mkafanyeni ziara kwenye maeneo yenu katika kutatua kero za Wananchi ili waondokane na Changamoto zinazowakabili kupitia uongozi wenu na tukifanya hivyo jamii itaishi kwa furaha na itaridhika na ifikapo mwaka wa uchaguzi hakutakua na maswali mengi kwa wagombea wetu." Mhe. Jichabu.
Dkt. Ntemi Kilekamajenga, Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ametoa rai kwa Wakuu hao wapya wa Wilaya kwenda kufanya kazi kwa weledi na kusaidia kutatua migogoro kwa Usuluhishi kwani jambo hilo likienda vema linapunguza kesi mahakamani ambazo pengine zingemalizwa kwenye ngazi za chini.
Ameongeza kuwa, Wakuu hao wa Wilaya wana wajibu pia wa kusimamia kwa dhati Kamati za Maadili za Wilaya kwani wao ndio wenyeviti wa kamati hizo ili kulinda maadili ya Utumishi na kupunguza malalamiko kwenye eneo hilo kutoka kwa wananchi.
"Waheshimiwa Wakuu wapya mlioapa leo nawaomba mkazingatie yote mtakayoahidi Umma na Viongozi waliopo hapa leo na vilevile mkazingatie Maadili yenu ya kazi katika kutekeleza majukumu yenu kwa Mujibu wa Sheria, Kanuni na Maadili." Amesema Jaji Godson Kweka wakati akitoa Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Wakuu hao wapya.
Baada ya Kiapo hicho Mhe. Rahel Kasanda, Mkuu wa Wilaya ya Magu amemshukuru Mhe. Rais kwa Uteuzi wake na ametumia wasaa huo kuahidi ushirikiano kwa viongozi na kwamba atahakikisha anafikisha huduma za kijamii kwa wananchi wa Magu na kutekeleza kwa asilimia 100, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/25.
"Kwangu mimi Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amenikopesha imani na sina budi kwenda kumuwakilisha kwa Uongozi uliotukuka na nina wajibu wa kutekeleza Ilani ya CCM na ninaahidi kwenda kusimamia haki kwa Wananchi wa Ukerewe." Amesema, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mhe. Hasaan Bomboko.
Katika wakati mwingine, Mhe. Shigela amekabidhi Pikipiki 230 zilizotolewa na Serikali kwa Maafisa Ugani mkoani humo na amewataka maafisa hao kwenda kuvitumia vitendea kazi hivyo kuwafikia wananchi ili kuongeza uzalishaji wa chakula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.