WANAHABARI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA KURIPOTI TAARIFA BINAFSI
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania (PDPC) Dkt. Emmanuel Mkilia amewataka waandishi wa habari kuzingatia sheria ya Tume hiyo katika kutoa taarifa binafsi za wananchi ili kulinda utu na faragha.
Dkt. Mkilia ametoa rai hiyo leo Jumamosi Machi 22, 2025 wakati akifungua mkutano na semina ya Waandishi wa Habari ambao tume hiyo imewaandalia ili kuwajengea uwezo juu ya majukumu ya tume hiyo nyeti.
Amesema, kuna madhara ya kijamii na hata kiuchumi endapo faragha za mtu zitazagaa bila ya ruhusa yake hivyo ni wasaa mzuri sasa wanahabari kufahamu sheria iliyoanzisha Tume hiyo na kuzingatia.
Ameongeza kuwa, pamoja na changamoto za kidigitali ambazo zinakuja kwa kasi Duniani kote bado wanahabari na wananchi wote wana wajibu wa kulinda siri za mtu ili kulinda utu wake pasipo kuathiri biashara ya kimtandao.
“Tumekuja Mwanza pamoja na mambo mengine tumekuja kuwajengea uwezo taasisi mbalimbali ili wapate uelewa wa sheria iliyoanzisha tume hii mwaka 2022 kwa sheria namba 11 na ikaanza kazi rasmi Mei 01, 2023 pamoja na uelewa wa ujumla wa ulinzi wa taarifa binafsi.” Dkt. Mkilia.
Akiwasilisha mada ya asili ya tume hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza upo chini kwa taasisi zake kujisajili kwenye mfumo wa tume hiyo na kwamba hali hiyo inatoa kiashairia kwamba Taarifa za watu bado haziko salama.
Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza huku ikilenga kutoa fursa kujifunza na kujengeana ulewa wa kina jinsi ya kulinda faragha za watu katika kazi za habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.