WANANCHI KUTOKA MIKOA YA KANDA YA ZIWA KARIBUNI KUMPOKEA MHE.DKT. SAMIA-RC MAKALLA
*Awahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi Tamasha la Bulabo litakalo funguliwa na Chifu Hangaya*
*Awaomba wananchi kumpa mapokezi makubwa kuanzia uwanja wa ndege na kwingineko*
*Wananchi wajitokeze na kumlaki akitembelea Miradi ya Daraja la JP Magufuli,Meli ya Mv Mwanza na kitega uchumi cha NSSF*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA. Amos Makalla amewaalika viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ziara yake ya kikazi Mkoani humo inayoanza Juni 12 hadi 15, 2023.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema hayo leo Juni 11, 2023 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wakati akizungumza waandishi wa habari juu ya ujio wa Mkuu huyo wa nchi katika ziara yake ya siku 3 mkoani humo.
"Rai yetu kwa viongozi na wananchi kujitokeza kwa wingi Juni 12, 2023 katika kumpokea Mhe. Rais akiwasili uwanja wa ndege na kumlaki kwa wingi barabarani akipita kuelekea Ikulu," CPA. Makalla
"Niwaalike wananchi kujitokeza kwa wingi kuja kwenye Tamasha la Utamaduni (Bulabo) ambapo Chief Hangaya atashiriki katika Tamasha hilo ambalo maandalizi yameshakamilika na Machifu na Watemi kutoka maeneo mbalimbali wameshawasili na atakagua Makumbusho ya Kiutamaduni Bujora pia kutakuwa na vikundi mbalimbali vya ngoma kutoka maeneo tofauti,"amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa
Aidha Mhe. CPA. Makalla amesema Juni 14, 2023 Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakagua miradi ya maendeleo na atapata fursa ya kuwasalimia wananchi katika miradi yote atakayopita kukagua.
"Nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi tumepata fursa ya kutembelewa na Mhe. Rais tujitokeze kwa wingi kushuhudia na kushirikiana nae katika Ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambapo atakagua daraja la JP Magufuli lililopo Kigongo Busisi na atapata fursa ya kuwasalimia wananchi wa Wilaya za Misungwi na Sengerema pia atakagua ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza HAPA KAZI TU pia atapata fursa pia ya kuwasalimia wananchi wa Wilaya ya Nyamagana baada ya hapo atakagua ujenzi wa Hoteli yenye hadhi ya nyota tano inayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)," Amesema Mhe. Makalla
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anahudhuria Tamasha la Utamaduni la (Bulabo) ambapo ndipo alipotawazwa kuwa Chifu Mkuu na kupewa jina la Chifu Hangaya Mwaka 2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.