Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa amewaagiza Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na taasisi zingine walio kwenye mnyororo wa Usafirishaji kuweka mfumo rahisi wa kuhamisha mizigo kutoka kwenye Meli kwenda kwenye reli ili kufanya gharama kuwa rafiki.
Ametoa agizo hilo leo alhamisi (Januari 19, 2023 alipofika kwenye kambi ya Fella Mkoani Mwanza akiwa kwenye ziara ya kukagua Mradi wa Reli ya Kisasa Standard Gauge Railway (SGR) kipande cha kuanzia Isaka-Shinyanga hadi Mwanza (KM 341) kinachogharimu Trilioni 3.06 ili kuona maendeleo ya Ujenzi.
Amesema, ni lazima kabla ya mwezi Mei 2024 ambapo kinatarajiwa kukamilika kipande hicho wataalamu wawe na mpango wa urahisishaji wa maunganisho ya kupokea mizigo kutoka kwenye Meli ili kushusha gharama na sio kutegemea matumizi ya mitambo ya kushushia pekee.
"Mkandarasi huyu (China Civil Engineering Construction Corporation) anafanya vizuri, na seksheni ya pili na ya tatu zinaendelea vizuri zaidi maana wameshaanza kutandika Reli na kwa ujumla tumefikia asilimia 23 Isaka - Mwanza na kwenye Ujenzi wa tuta tumefikia asilimia 56, sisi kama wizara tunakwenda kusimamia kwa umakini ili mradi huu uende kama ilivyotarajiwa."
Vilevile amesema Wizara itaendelea kusimamia ujenzi wa reli hiyo kwa uzalendo na kwamba wamejipanga kumaliza kabisa tatizo la wizi wa vifaa vya ujenzi kama Mafuta, Nondo na Diseli ili kufanya Mradi huo kwenda kwa haraka lakini kwa ubora uliokusudiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amemshukuru Mhe. Rais kwa Waziri kwa ukaguzi wa Miradi ya Kimkakati Mkoani humo ikiwepo Ujenzi wa Jengo la Kisasa la Abiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Meli ya MV Mwanza na Daraja la Kigongo Busisi ambayo inatarajiwa kuwainua wananchi kiuchumi.
"Huu Mradi unawapa heshma kubwa sana watanzania, zoezi tu la treni kupita kwenye daraja la juu kwenye eneo hili (Mkuyuni-Mjini Mwanza) unaupa hadhi kubwa Mkoa lakini pia unaokoa fedha kwa kutohusisha kuvunja nyumba za wananchi na kuwalipa fidia ili kupisha Ujenzi wa Reli." Mhe. Malima.
Mkurugenzi wa Shirika la reli nchini Masanja Kadogosa amesema Ujenzi unaendelea vizuri na kwakua kuna soko kubwa la usafirishaji mizigo kutoka Uganda kwa kutumia ziwa Viktoria, Shirika hilo limejiiandaa kutumia fursa hiyo kwa kutumia Bandari ya Mwanza pindi mradi utakapokamilika.
Amefafanua kuwa Shirika hilo limejipanga kuweka Miundombinu rafiki ya kurahisisha upakuaji wa mizigo kutoka kwenye Meli kwenda kwenye Reli katika pande zote mbili za bandari kwani kutakua na mapokeo ya reli yenye uwezo wa hadhi zote wa uhamishaji wa mizigo.
Kwa mujibu wa Ndg Kadogosa, abiria kwenda Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma hawatahitaji kufika katikati ya mji ili kuendea na safari kwani katika eneo la Stesheni ya Fela kutakua na kituo cha mabasi kama sehemu ya mradi ambayo itawezesha abiria kuendelea na Safari kupitia nje ya Mji huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.