Leo Juni 03, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe Mhandisi Robert Gabriel amekagua ujenzi wa barabara ya Kisesa-Kayenze wilayani Magu yenye urefu wa KM 10 inayogharimu Tshs Milioni 134 kiwango cha Changarawe ambapo amemuagiza Mkandarasi kukamilisha kwa wakati na kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuimarisha mitaro ya maji ili iweze kudumu muda mrefu.
Akikagua Mradi wa Vyumba vinane vya madarasa vilivyotekelezwa kwa Tshs. Milioni 160, Mhe.Mhandisi Gabriel kwenye shule ya Sekondari Lugeye ametoa rai kwa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na kufanya mazoezi ya viungo ili waweze kufaulu kwenye mitihani yao.
"Kwanza mtangulizeni Mungu, pili epukeni tabia mbaya ya mahusiano shuleni, someni kwa bidii mtafanikiwa huu ni wakati wa kutengeneza maisha yako tena somo la hesabu lipeni kipaumbele." Mkuu wa Mkoa.
Mwanafunzi Melesiana Sylivester wa Kidato cha nne katika shule ya Sekondari Lugeye ajipatia zawadi ya papo hapo zaidi ya Shilingi elfu 60 kutoka kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa baada ya kujibu vizuri swali la somo la Hesabu alipoulizwa njia zinazotumika kukokotoa 'simultaneous equation'.
Vilevile, Mhe Mkuu wa Mkoa amefanya ziara kwenye Mradi wa Maji ya bomba Kahangara wenye thamani ya zaidi ya Milioni 500 huku ukitarajiwa kuwahudumia zaidi ya watu 9600 ambapo amewapongeza RUWASA kwa utekelezaji wa mradi huo ambao utawapunguzia wananchi umbali wa kutembea kutafuta huduma hiyo na upatikanaji wa maji salama utapanda hadi 86% kutoka %34 za hivi sasa kwenye eneo hilo.
Aidha, Mhandisi Gabriel amekagua mradi wa jengo la X-RAY na Ultra Sound wenye thamani ya Milioni 66.2 katika Kituo cha Afya Kahangara na amesisitiza marekebisho kwenye dosari chache zilizobainishwa ili mradi uwe nadhifu na uweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Naomba mazingira ya shule hii yawe vizuri na rafiki kwa kutolea elimu kwa watoto wetu, hakikisheni kule nje kote kunakua sawa" Amesema Mkuu wa Mkoa wakati wa kukagua mradi wa ujenzi wa shule ya Msingi Bugomba kwa zaidi ya Milioni 89.
Milioni 90 zinazotekeleza ujenzi wa nyumba 3 za watumishi hospitali ya Magu zimemfikisha Mhe. Mkuu wa Mkoa kwenye mradi huo ambapo ameagiza ukamilishwaji wa kujibana ili fedha hizo ziweze kusaidia kuboresha mambo mengine kwenye mradi huo kama kupata makabati au matanki ya maji kwenye nyumba hizo tatu za mfumo wa pamoja.
Mhe.Mhandisi Gabriel amekagua pia mradi wa kampeni ya Lishe, Ziro Malaria na kampeni ya VVU/UKIMWI katika hospitali ya wilaya Magu na ametoa wito kwa wananchi kula vyakula vyenye lishe bora katika kujikinga na maradhi mbalimbali na kuzingatia usharudi wa kitaalamu kujikinga na maambukizi ya Malaria na VVU/UKIMWI.
Aidha, amebainisha kuwa ni lazima Halmashauri ishiriki kutokomeza Matatizo ya utapiamlo kwa watoto kwa kushirikiana na wataalamu wa masuala ya lishe kwa kupanga na kutoa fedha kwenye sekta hiyo muhimu kwa amendeleo ya ustawi endelevu.
Mradi wa Anuani za makazi umebainisha kuwa Nguzo za Majina ya mitaa na Barabara wilayani humo umefikia zaidi ya asilimia 50 na ndipo Mhe.Mkuu wa Mkoa akatoa wito kwa watendaji wa zoezi hilo kuwa wabunifu ili kutumia Rasilimali chache zilizopo kukamilisha zoezi hilo nyeti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.