WANANCHI WA KISESA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUWAJENGEA SHULE MPYA
Wananchi wa Kata ya Kisesa Wilayani Magu wamempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule mpya ya awali na msingi kwenye kijiji cha Idugija iliyogharimu kwa zaidi ya Tshs. Milioni 540 kupitia mradi wa BOOST.
Akizungumza leo Septemba 18, 2024 kwa niaba yao, Diwani wa kata ya Kisesa Mhe. Marco Kabadi amesema shule hiyo imekuja kuondoa changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule ya msingi Kisesa na kuwaepusha na ajali zilizosababishwa na kuvuka barabara.
Akizungumza wakati akikagua huduma na majengo kwenye shule hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali ya awamu ya sita iko imara na itaendelea kutatua changamoto za wananchi ikiwemo na kuwaletea maji na umeme kwenye shule hiyo ambapo iliainishwa kama changamoto shuleni hapo.
Aidha, Mhe. Mtanda amewataka wazazi kuwapa malezi bora watoto wao na kuhakikisha wanasimamia elimu ili kupata kizazi bora na chenye uzalendo kwa Taifa lao pamoja na kuendelea kulinda amani ya Taifa ili kupata maendeleo.
Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Benifaxad Chiguru amesema shule hiyo mpya ina vyumba 16 vya madarasa, matundu 24 ya choo, jengo la utawala, ofisi 4 za walimu, madawati 210, viti 30 na meza 30 na ina jumla ya wanafunzi 1511.
Akiendelea na ukaguzi wa miradi ya elimu, Mkuu wa Mkoa amewatembelea watoto 18 wenye mahitaji maalumu kwenye Shule ya msingi Wita na akamuagiza Mkurugenzi Mtendaju wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu kuwaongezea vyerehani watoto hao pamoja na kuboresha miundombinu ili iwe rafiki.
Katika hatua nyingine Mhe. Mtanda amewahimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa zoezi litakalofanyika kuanzia Oktoba 11-20 pamoja kushiriki zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 27, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.