Rai imeendelea kutolewa kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake kuchangamkia fursa ya Maadhimisho wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza inayoendelea uwanja wa CCM Kirumba ili waelimike kuhusiana na afya ya mwili kwa ujumla.
Akifungua leo maonesho na utoaji wa huduma za afya,Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Ndugu Kaspar Mmuya amesema kasi ya magonjwa hayo sasa imefikia asilimia 40 huku waathirika wakianzia watu wenye umri mdogo tofauti na miaka ya nyuma maradhi hayo yalikuwa yakiwakuta wazee hali hiyo inatoa somo kuwa tatizo hilo ni kubwa hapa nchini.
"Wananchi wanapaswa sasa kuzingatia njia sasa za kuboresha afya zao kuanzia mlo sahihi wa vyakula visivyo na mafuta sana pamoja na chumvi na kula kwa wingi mboga za majani na matunda"amesema Mmuya.
Mtendaji huyo mwandamizi wa Serikali amesema takwimu zinaonesha watu hawana utaratibu wa kuchunguza afya zao na wanapogundulika tatizo linakuwa limepiga hatua hali ambayo inaleta hofu na taharuki.
"Tukiwa na tabia ya kujichunguza afya mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha,nguvu kazi ya Taifa itakuwa imara lakini kinyume cha hapo kasi ya kiuchumi kuanzia ngazi ya familia itazorota kutokana na muda mwingi na gharama kutumika kujitibu" amesisitiza Naibu Katibu Mkuu
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa magonjwa yasiyoambukiza,ajali na afya ya akili kutoka Wizara ya Afya Dkt James Kiologwe amesema mwamko uliooneshwa na wananchi tangu kuanza kwa wiki hiyo unawapa matumaini kuwepo na matokeo chanya katika malengo yaliyokusudiwa.
Kilele cha Maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yatakuwa Novemba 12 mgeni rasmi akitarajiwa kuwa ni Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.