Wananchi wa Mwanza wameendelea kukumbushwa kushiriki vyema zoezi la Sensa na Makazi ya Watu litakalofanyika Kitaifa Agosti 23 mwaka huu bila kuwaficha watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel akifungua kikao leo cha Kamati ya Mkoa ya Sensa ya Watu na Makazi kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa amesema kila mwananchi anatakiwa kuhesabiwa ili kurahisisha mipango ya Maendeleo ya nchi.
"Kamati hii ya Mkoa naomba tuwe mabalozi wazuri wa kuelimisha Wakazi wa Mwanza kuhusu kushiriki zoezi hili wakiwemo ndugu zetu wenye Ulemavu wasifichwe nao wana haki ya kuhesabiwa" amesisitiza Mhe Gabriel
Amesema, wananchi ni lazima wahamasishwe na kuelimishwa mara kwa mara ili watambue ni kwa faida yao kuhesabiwa kwani Serikali itakapopanga mikakati ya Maendeleo kama Elimu, Afya na Maji itawahusu wao moja kwa moja.
Mratibu wa Sensa Mkoa Goodluck Lyimo amesema maandalizi ya zoezi hilo yanakwenda vizuri ikiwemo kutengwa maeneo ya kuhesabia na kwamba kwenye Halmashauri za Misungwi na Ukerewe likiendeshwa na Wataalamu wa ramani kutoka Ofisi ya Taifa Takwimu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike amesema wamejipanga vizuri kwenye Halmashauri zote za Mkoa kuhakikisha Makundi yote yameelimishwa vyema kuhusu Sensa hiyo.
Sensa ya Watu na Makazi itafanyika nchi nzima Agosti 23 mwaka huu kwa watu waliolala ndani ya mipaka ya Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.