WANANCHI WAELIMISHWE VIZURI KUHUSU UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA: M/KITI WA TUME
Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele ametoa wito kwa wadau kuwaelimisha wananchi ili waweze kushiriki kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura kama msingi wa uchaguzi bora wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Ametoa wito huo leo Agosti 9, 2024 Mkoani Mwanza wakati akifungua mkutano wa Tume hiyo na wadau uliofanyika uliolenga kupeana taarifa mbalimbali ikiwemo kuandikisha wapiga kura wapya, uboreshaji wa daftari pamoja na hatua za maandalizi kama ununuzi.
"Ndugu wadau, kama nilivyo sema hapo awali nchi yetu inakwenda katika uchaguzi mkuu hapo mwakani, zoezi hili la uboreshaji tayari limezinduliwa mkoani Kigoma Julai 20, 2024 na Mhe.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,huu ni mzunguko wa tatu kwa Mkoa wa Mwanza na Shinyanga utakaoanza Agosti 21 hadi 28 mwaka huu" ,amesema Mhe.Mwambegele
Vilevile amefafanua kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kujiandikisha mara mbili kupiga kura na adhabu yake ni kifungo kisichozidi miezi 6 au kisichozidi miaka miwili au faini ya Tshs laki moja au isiyo zidi laki tatu hivyo ni vyema wananchi wakaelimishwa vizuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume hiyo ambaye pia ni Katibu wa Tume Bw. Ramadhan Kailima amesema kwa Mkoa wa Mwanza wanatarajia kuwa na wapiga kura wapya 190,131 sawa na ongezeko la asilimia 10.3 la wapiga kura 1,845,816 waliopo sasa.
Makundi mengine yanayoshiriki mkutano huo ni Maafisa Habari ngazi ya mkoa na Halmashauri, wahariri wa vyombo vya habari, vijana, wazee, wanawake, walemavu pamoja na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na harakati za maendeleo kwa wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.