Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima amewataka wananchi wanaozunguka kulinda chanzo cha Maji Ziwa Victoria Ihelele kwenye Kijiji cha Nyangomang'ho kata ya Ilujamate kutunza chanzo hicho kinachohudimia wananchi takribani 1,250,000 (2021) kwenye Mikoa mitano.
Akikagua Mradi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama-Shinyanga (KASHWASA) unaozalisha takribani mita za Ujazo 63,000 kwa siku, leo Machi 02, 2023 Mhe. Malima amesema jamii ina wajibu wa kuutunza mradi huo kwa dhati na kujiepusha na shughuli za kiuchumi zinazochafua Maji na kuharibu mazingira.
"Huu mradi ni wa kitaifa, watanzania wengi wanapata maji kutoka hapa Ihelele, siku za nyuma nilipata kusikia kuwa Maji yanayotumika Tabora yanatoka kwenye Chanzo cha Ihelele na leo nimefurahi kufika hapa na kuuona mradi huu kwa macho yangu mwenyewe." Malima.
Mkurugenzi wa Bonde la Ziwa Victoria Mhandisi Renatus Shinhu amesema taasisi hiyo imepanda Zaidi ya Miche ya Miti elfu 8 na kwamba pamoja na afua zingine wametumia Zaidi ya Milioni 250 kuhifadhi mazingira ya bonde hilo na imesadia kuongeza ubora wa Maji na kurejesha na uoto wa asili ambao ulianza kutoweka.
"Chanzo hicho kinakabiliwa na uharibifu wa Mazingira ukiwemo ufugaji wa kilimo ndani ya hifadhi, ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, uchomaji wamkaa na matofali na uvuvi wa samaki usio endelevu na kwamba hayo yanasababisha uchafuzi wa chanzo na kupelekea kuongezeka kwa gharama za kutibu Maji." Mhandisi Shinhu.
Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa ziwa Victoria lina ukubwa wa Kilomita za Mraba 68,800 na kwa upande wa Tanzania ni 35,700 na kwamba ziwa hilo lima Maji kiasi chan Mita za Ujazo Bilioni 2,700 na ka upande wa Tanzania ni Bilioni 1,400.
Naye, Mkurugenzi wa Mamlaka ya majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama-Shinyanga (KASHWASA) Mhandisi Patrick Nzamba amefafanua kuwa chanzo hicho kina uwezo wa kuzalisha Lita Milioni 80 hadi 120 kwa siku na kwamba kwa sasa wanazalisha Lita Milioni 63 na kwamba gharama kubwa za uzalishaji na wateja kutolipa kwa wakati Ankara zao zinaathiri uendeshaji wa mradi.
Chanzo cha Maji ziwa Victoria Ihelele kinatumiwa na Mamlaka ya KASHWASA kusambaza Maji katika Mamlaka zilizopo katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Tabora, Singida na Simiyu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.