WANANCHI WANAOTAKIWA KUFIDIWA KUPISHA UWANJA WA NDEGE MWANZA WATAKIWA KUWA NA SUBIRA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewasihi Wananchi wa mitaa mitano iliyoko katika Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza wanaokabiliwa na mgogoro wa mpaka wa uwanja wa ndege kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kutafuta suluhu.
Mhe. Mtanda ameyasema hayo leo Februari 21, 2025 alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Mitaa hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Nyamilolelwa na kuwataka kuendelea kuwa wastahimilivu wakati Serikali ikiendelea na uchakataji wa upatikanaji wa suluhu.
Mkuu wa Mkoa amefanya mkutano huo ikiwa ni mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela kuuliza swali bungeni la ni lini serikali itawalipa fidia wakazi wa mitaa mitano ya kata ya Shibula ambapo majibu ya Waziri wa ardhi alisema kuwa wananchi hao wapewe viwanja mbadala kauli iliyozua utata na mkanganyiko baina ya wahanga hao.
Akuzungumza na Wanachi hao, Mkuu wa Mkoa amesema Serikali inaendelea na mchakato wa majadiliano ili waje na uamuzi sahihi ambapo kwa siku ya leo yeye pamoja na Kamati ya Usalama Mkoa wameamua kuja uwandani kwa lengo la kujionea eneo la mgogoro wawe na uelewa wa pamoja ili waweze kuishauri Wizara na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo.
Mimi kama Mkuu nimeona ni lazima niende na kamati yangu ya usalama kutembelea uwandani, wote hapa tulikuwa hatujafika eneo la mgogoro na ninatambua tayari kuna tathmini kadhaa zimeshafanyika ikiwemo ile ya kwanza ya shilingi bilioni 19, tathmini ya pili ya bilioni 26 nimekuja kuwaomba endeleeni kuwa wastahimilivu. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Aidha Mkuu wa Mkoa amesema kama Serikali ya Mkoa haijapokea taarifa kamili ya maandishi kuhusu uamuzi wa kauli hiyo iliyotolewa na Waziri wa ardhi hivyo wataendelea kujadiliana na kusubiri tamko rasmi la kimaandishi.
“Tunaendelea kutafuta ufumbuzi wa jambo hili na kwa kuwa tayari tumeshakusanya maoni yenu, na maoni yenu yote matano mliyotupatia, tupeni muda kama serikali ili tuweze kushauriana vizuri na tuje na muafaka”.
Mgogoro huo wa mipaka ya uwanja wa ndege Mkoa wa Mwanza umedumu kwa takribani miaka 8 sasa ambapo Mkuu wa Mkoa amesema yuko tayari kuhakikisha Serikali inaumaliza mgogoro huo kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sikivu na watafikia maamuzi ambayo ni sahihi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.