Wananchi wa Kijiji cha Kabila, wilayani Magu wamesema serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu ya afya ukiwemo uboreshaji wa Kituo cha Afya Kabila na hivyo kuomba iwaongezee watumishi na dawa ili kwenda sambamba na utoaji wa huduma.
Walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana walipozungumza na Uhuru baada ya Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Magu kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya, maji, elimu na umeme ukiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
Mmoja wa wananchi hao Leonila Gima, kwa niaba ya wenzake alisema,serikali imefanya jambo la jema la kukipanua na kukiboresha kituo cha Afya Kabila lakini kinakabiliwa na uhaba wa watumishi na dawa, hivyo waongeze ili kuboresha utoaji wa huduma za matibabu.
“Serikali kutoa fedha za kuboresha kituo hiki tunaishukuru sana,changamoto kubwa ya kituo hiki kwa sasa ni wataalamu wachache pamoja na dawa,serikali iongeze wataalamu hao ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji na utoaji huduma kwa wananchi,”alisema Gima.
Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya,kilichofanyiwa upanuzi mkubwa kwa sh. milioni 400 Dk.Bijengo Mabiba,alikiri kuwapo uhaba wa watumishi wa kada zote, hivyo kuzorotesha utaoji wa huduma.
“Kulingana na ukubwa wa kituo hiki kilichopo pembezoni wagonjwa ni wengi,tupo madaktari 5 wakiwemo teachnicina wawili, mahitaji ni 4 pia na wauguzi waliopo ni 7 mahitaji ni 9 ili kuboresha utendaji na utoaji huduma kwa wananchi,”alisema.
Dk. Mabiba aliiambia Kamati ya Siasa kuwa Septemba 2020 walipokea sh.milioni 400 za ujenzi wa miradi miwili ya matundu 8 ya vyoo na majengo 5 ya upasuaji,nyumba ya mganga,stoo ya dawa, wodi ya wazazi,maabara na chumba cha kuhifadhi maiti.
Alisema ili kukamilisha mradi mkubwa wa miundombinu ya majengo hayo matano yaweze kuanza kazi ya kutoa huduma kwa wananchi Mei mwaka huu,zinahitaji sh.milioni 48.
Mganga mafawidhi huyo alifafanua fedha hizo ni za ununuzi wa milango 66,bawaba,masinki mawili ya maji kwenye wodi ya wazazi na chumba cha upasuaji,mabomba,manteki ya maji na kufunga umeme kwenye mashine ya kusukuma maji.
Kutokana na maelezo hayo Kamati ya Siasa kupitia kwa Mwenyekiti, Zablon Makoye iliuagiza uongozi wa kituo hicho cha afya kwa vile hakuna nguvu za wananchi, wajitahidi mradi huo ukamilike ili utoe huduma haraka kwa wananchi.
Aidha kamati hiyo ikiwa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Wilaya ya Magu,linalojengwa kwa sh. milioni 380 iliagiza uboreshaji wa haraka ufanyike, umakini,uangalifu na usimamizi uongezwe ili kuepuka kuingizia serikali hasara.
Awali Katibu wa Hospitali hiyo Wilaya ya Magu, Saada Musa, alisema fedha za ujenzi wa jengo zilitolewa na Global Fund, Serikali Kuu na Halmashauri,hivyo zinahitajiika sh.milioni 10 za kukamilisha miundombinu ya jengo ili lianze kutumika kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuletea fedha za kujenga OPD na kuimarisha miundombinu ya afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya wananchi bila vikwazo,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.