WANANCHI ZAIDI YA ELFU 12 WAPATA HUDUMA YA MAJI SAFI
*Mkuu wa Mkoa amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha zaidi ya Bilioni 1.7 kujenga mradi huo*
*Awasihi wananchi kulinda na kutunza mradi huo*
*Ametoa rai kwa Jumuiya ya watumia Maji kuumiliki mradi huo*
*Aahidi upanuzi wa Mradi huo kadiri watu wanavyoongezeka*
*Amtaka mkandarasi kuongeza nguvu na watendaji kusimamia Ujenzi wa jengo la Halmashauri*
*Amewataka watumishi wa idara ya afya kuwatumikia wananchi kwa lugha ya Staha*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Novemba 03, 2023 amefika wilayani Magu akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi kwenye halmashauri zote za mkoa huo.
Akikagua mradi wa Maji wa Bugando-Chabula unaotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 1.7 na Wakala wa Maji vjijini (RUWASA) Mhe. Makalla amewataka wananchi kuulinda mradi huo uwapatie huduma hiyo muhimu ya kijamii kwa muda mrefu.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kwani wananchi zaidi ya elfu 12500 watanufaika na huduma ya Maji hayo kutoka vijiji Vinne vya Bugando, Chabula, Nyashigwa na Kongolo kwenye kata za Chagula na Kongolo.
"La kwanza tulinde chanzo hiki cha maji, la pili jumuia ya watumia maji mtoe ushirikiano kwa kukarabati mambo madogo madogo na muumiliki wenyewe mradi wenu kwani kuna uhitaji wa upanuzi wa mradi huu kutokana na ongezeko la wananchi hivyo wakati ukifika pawe salama." CPA Makalla.
Awali, Kaimu Meneja wa RUWASA Magu Mhandisi Daud Amlima alifafanua kuwa mradi huo wa chanzo cha Ziwa Viktoria umefungwa pampu yenye uwezo wa kusukuma lita elfu 75 kwa saa kwenda kwenye tanki la lita 250,000 na kwamba kuna vituo vya kuchotea maji 31.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chabula, Masatu Mgaya ametumia wasaa huo kuwashukuru Serikali kwa mradi huo na ameomba mamlaka husika kufikisha maji kwenye maeneo ambayo bado haujawafikia wananchi kwani awali walikua na shida kubwa ya maji kwenye vijiji hivyo.
Akikagua ujenzi wa Jengo la Halmashauri linalojengwa kwa awamu kwa zaidi ya Bilioni 7.5 ambapo limefikia hatua ya umaliziaji kwa asilimia 85 Mhe. Makalla amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo ambao umetumia zaidi ya miaka 10 ili Mkurugenzi mtendaji na watumishi wahamie.
"Nampongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kututatulia adha ya fedha kwani sasa tumeletewa tena kwa ajili ya ukamilishaji, nina imani jengo hili litakamilika kwa wakati na Halmashauri na watendaji wake watapatikana hapa na wananchi watapata huduma nzuri kwenye jengo hili ambalo litakua la mfano kwenye mkoa wetu." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Baadae Mhe. Mkuu wa Mkoa alikagua mradi wa maji Nyag'hanga-Iseni uliofikia asilimia 75 ya utekelezaji na amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo ifikapo tarehe 31 Disemba 2023 ili wananchi zaidi ya elfu 31 kutoka kwenye vijiji vitano wanufaike na maji safi na salama kupitia mradi huo unaojengwa kwa zaidi ya Bilioni 5.
Vilevile, amekagua mradi wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa Shilingi Milioni 750 na kuridhishwa na ujenzi huo wa Jengo la Uzazi na Upasuaji kwa wanaume na ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo na za kununua vifaa tiba zaidi ya Milioni 500 pamoja na magari ya kubeba wagonjwa.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwataka watumishi wa idara ya afya kuwajibika katika kuwatumikia wananchi kwa lugha nzuri, staha na kutunza Miundombinu pamoja na vifaa tiba na kujiepusha na tabia hatarishi kwenye ustawi wa sekta ya afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.